Halmashauri ya Jiji la Dar Es Salaam kupitia Idara ya Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii imetoa elimu juu ya kuzingatia lishe kwa kina mama wajawazito katika Kituo cha Afya Kinyerezi, ikiwa ni sehemu ya kutekeleza mpango wa kutoa elimu ya lishe kwa mama wajawazito na watoto katika Kata 36 na Mitaa 159 ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.
Akiongea katika mafunzo hayo, Diwani wa Kata ya Kinyerezi Mhe. Leah Mgitu amesema Serikali ya Tanzania imedhamiria kuendelea kulipa umuhimu wa kipekee suala la lishe nchini ili kuhakikisha Tanzania inakuwa na uchumi imara kupitia maendeleo ya viwanda kwani Maendeleo ya Taifa pamoja na mambo mengine, yanahitaji uwepo wa watu (nguvu kazi) wenye afya njema na lishe bora ili kuwawezesha kufanya kazi kwa bidii na Kuchochea maendeleo ya nchi.
"Ili mtoto aweze kuwa na utulivu darasani na awe vizuri kitaaluma lazima mzazi uzingatie lishe kwa mtoto wako na iwe ni kipaumbele chako." Ameongeza Mhe. Mgitu.
Akitoa mafunzo hayo ya lishe Afisa Lishe wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Bi. Neema Mwakasege amesema “Lishe bora ni kula chakula cha kutosha na chakula chenye virutubisho vyote muhimu. Lishe bora husaidia mwili kukua vyema, kuujenga mwili lakini pia huimarisha kinga ya mwili ili kuweza kupigana na magonjwa. Ili lishe iwe bora ni muhimu iwe na mchanganyiko wa Makundi sita ya chakula ambayo ni protini, wanga, fati, mbogamboga, madini, matunda na maji kwa wingi hivyo tuhakikishe tunawapa watoto mlo kamili lengo likiwa ni kupunguza udumavu na kuongeza uelewa kwa watoto wetu kwani lishe bora ndio msingi wa makuzi ya kimwili kwa watoto hawa.
Hata kama tunaanda mlo kamili tusipoandaa kwenye mazingira safi itakua ni kazi bure hivyo inabidi tuhakikishe tunaandaa vyakula hivyo katika mazingira, tunahifadhi chakula sehemu safi na salama pamoja na kuchemsha maji ya kunywa ili tukinge afya za watoto wasiadhiriwe na magonjwa nyemelezi”.
Sambamba na hilo, Bi. Mwakasege amewahimiza wazazi/walezi kuhakikisha wanawapeleka watoto kliniki hadi watakapofikisha miaka 5 ili kuweza kujua hali zao huku akiwataka wazazi/walezi ambao watoto wao hawajapata chanjo ya Surua wahakikishwe wanawapeleka kituo cha afya kupata chanjo hiyo ili wasije wakalemaa.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.