Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Sipora Liana, amewaagiza watumishi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi baada ya kumaliza semina ya udhibiti wa vihatarishi katika sehemu za kazi.
Liana alitoa maagizo hayo Septemba 8, mwaka huu alipokuwa akifungua semina ya udhibiti wa vihatarishi katika sehemu za kazi inayofanyika kwa siku nne katika ukumbi wa mikutano wa Karimjee jijini Dar es Salaam.
Katika semina hiyo inayoendeshwa na wataalam kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Liana amewataka Wakuu wa Idara, Vitengo na wawakilishi wa watumishi wa Halmaahauri na Jiji na Mashirika yake kutambua umuhimu wa semina hiyo na kuyafanyia kazi mafunzo watakayopata.
"Watu wengi hawafamu kabisa kuhusu udhibiti wa vihatarishi sehemu za kazi, ninataka mwisho wa semina nanyi muwaelimishe pia watumishi wa ngazi za chini", alisema Liana.
Aliwaelekeza washiriki wa semina hiyo kuwa wasikivu, kuzingatia umuhimu wa mafunzo hayo na kusimamia utekelezaji wa mambo waliyofundishwa.
Washiriki wengine pia wa semina hiyo ni Mameneja, Wakuu wa Idara na Vitengo kutoka Shirika la Masoko Kariakoo, Shirika la Maendeleo na Uchumi Dar es Salaam (DDC) na Kituo cha Biashara cha Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam (Machinga Complex) ambavyo vyote ni vitega uchumi vya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.