Watumishi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam leo tarehe 10 Oktoba, 2023 wamepata mafunzo ya kujengewa uelewa wa Mfumo mpya wa Manunuzi ya Umma kwa njia ya Kielekroniki (National e-Procurement System of Tanzania - NeST) ambao umeanza kutumika rasmi tarehe 1 Oktoba, 2023 baada ya mfumo wa manunuzi wa zamani wa TANePS kufikia ukomo wake.
Akiongea na washiriki, mwezeshaji wa mafunzo hayo Bw. Sovela Shirima amesema "Mfumo huu wa NeST ni wa kizalendo kwani umetengenezwa na Watanzania na ni mfumo rafiki na rahisi kwa watumishi, na utasaidia kudhibiti rasilimali za Serikali lakini pia ni mfumo wa wazi na shirikishi kwani unaondoa mianya yote ya upendeleo na rushwa na umeunganisha Taasisi zote za Serikali pamoja na mabenki. Vilevile utarahisisha utendaji wa kazi za Serikali katika ushindani kwa wazabuni, uandaaji wa zabuni ndani ya mfumo na utaondoa matumizi ya karatasi (paper work) kwani kila kitu kitafanyika ndani ya mfumo."
Aidha, Afisa TEHAMA Bw. Mussa Luvanda ameeleza kua mfumo huo utasaidia Watumishi kupunguza muda wa utafutaji na upatikanaji na bidhaa kupatikana kwa muda mfupi kwani ni mwepesi na unaeleweka kwa watumishi na utasaidia kuandaa mpango kazi wa manunuzi kulingana na hitaji la Idara husika.
Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii Bi. Lilian Shoo amesema kuwa mfumo huu unawasaidia Watumishi kujua ni namna gani wataweza kuandaa taratibu zote za manunuzi, kwani mfumo unaelekeza ukifika kiasi fulani cha pesa utatakiwa kutangaza tenda na kiasi fulani utatumia rasilimali zilizopo.
Mwezi Julai, 2023 Serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) ilianzisha mfumo mpya wa manunuzi wa National e-Procurement System of Tanzania (NeST) ambao umeanza kutumika rasmi kuanzia tarehe 1 Oktoba, 2023 ili kukidhi mahitaji ya Nchi katika Manunuzi ya Umma na kukabiliana na changamoto za mfumo wa zamani wa TANePS uliofikia ukomo Septemba 30, 2023.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.