Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa kushirikiana na Chuo cha Serikali za Mitaa cha Hombolo kilichopo Mkoani Dodoma, wametoa mafunzo ya awali kazini kwa watumishi wapya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa lengo la kuwasaidia watumishi hao kupata uelewa wa kanuni na misingi ya Utumishi Ili kutimiza malengo ya Serikali.
Mafunzo hayo yametolewa leo tarehe 6 Oktoba, 2023 kwenye ukumbi wa Mikutano wa Arnatoglou ambapo Watumishi hao walifundishwa misingi na haki za mtumishi, misingi ya sheria katika kusimamia haki na wajibu kwa watumishi wa umma; miongozo na sera mbalimbali ya kuifuata katika utendaji wao wa kazi na namna bora ya kudumisha mahusiano mazuri katika maeneo yao ya kazi na watu wanaowatumikia.
Naye mratibu wa Mafunzo hayo Bi Arafa Mangungu amesema "Mafunzo hayo yatawasaidia watumishi wapya wa Serikali kujua sheria za kazi, kanuni, misingi na pia kujua haki zao kama Watumishi. Hivyo niwaase kuhakikisha mnatekeleza wajibu wenu kikamilifu kwa kufanya kazi kwa bidii, uadilifu pamoja na kuzingatia taratibu na kanuni za Utumishi wa Umma."
Kwa upande wake muwezeshaji wa mafunzo hayo Afisa TEHAMA kutoka Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo Ndg. Kassim Halfani amewataka watumishi hao kujisajili kwenye Mfumo wa Ujifunzaji Kielektroniki - MUKI ili kupata mafunzo mbalimbali yanayohusiana na Muundo wa Serikali za Mitaa na Utumishi wa Umma kwa ujumla.
Aidha, Bi Joyce Elias ambaye ni mshiriki wa mafunzo hayo, amesema mafunzo waliyopata yamewasaidia kujua yale yanayopaswa kufanywa na yasiyopaswa kufanywa wawapo kazini na kuahidi kwenda kuwa Watumishi bora wa Umma.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.