Na: Hashim Jumbe
TIMU ya UMITASHUMTA Wilaya ya Ilala, leo tarehe 21 Julai, 2022 wameibuka Mabingwa wa Jumla wa Mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) ngazi ya Mkoa wa Dar es Salaam, yaliyofanyika kwa Siku Tano (5) katika viwanja vya Benjamini Mkapa na Uhuru vilivyopo Temeke, Dar es Salaam.
Mashindano hayo yaliyoshirikisha Timu Tano (5) kutoka katika Wilaya za Mkoa wa Dar es Salaam ambazo ni Wilaya ya Ilala, Kinondoni, Ubungo, Kigamboni na Temeke yalianza tarehe 17 Julai, 2022 na kughairishwa Siku ya leo na Afisa Elimu Mkoa wa Dar es Salaam, Ndugu Abdul Maulid, huku Timu ya Wilaya ya Ilala wakiibuka washindi wa Jumla kwa kubeba Jumla ya Vikombe Kumi na Moja (11) ambapo Vikombe Nane (8) ni vya nafasi ya kwanza, Vikombe Viwili nafasi ya Pili (2) na Kikombe Kimoja (1) Ushindi wa Jumla na Nafasi ya Pili ilienda kwa Timu ya Wilaya ya Kigamboni.
Aidha, mashindano hayo yaliwakutanisha jumla ya wanamichezo 600 walioweka kambi Shule ya Sekondari Jitegemee, ambapo Afisa Elimu Mkoa wa Dar es Salaam, Ndugu Abdul wakati anaghairisha mashindano hayo aliwaasa wanafunzi hao kuendelea kucheza michezo mbalimbali
"Kwa namna yoyote ile watoto muhakikishe mnacheza michezo hii kila siku kwa sababu michezo hii inajenga afya na vile vile michezo ni ajira, siyo kila mtoto atafaulu physics, siyo kila mtoto atafaulu English, lakini mwengine atafaulu katika michezo, kwa hiyo tuiendeleze michezo"
Pamoja na Timu ya Wilaya ya Ilala kushinda Ubingwa wa Mkoa, lakini pia imeweza kutoa wachezaji wengi zaidi kwenda timu ya Mkoa wa Dar es Salaam, wachezaji 73 kati ya wachezaji 120 wanaounda timu ya Mkoa wa Dar es Salaam itakayokwenda kushiriki michuano hiyo kwa ngazi ya Kitaifa, mashindano yatafanyika Mkoani Tabora kuanzia tarehe 29 Julai, 2022
Itakumbukwa kuwa timu ya Wilaya ya Ilala ndiyo walikuwa Mabingwa watetezi wa michuano hiyo kwa Mkoa wa Dar es Salaam na mwaka huu wameweza kutetea tena ubingwa wao na kuwa Mabingwa kwa Miaka Sita (6) mfululizo
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.