Wilaya ya Ilala yaweka mikakati ya kudhibiti Magonjwa ya Mlipuko katika Jamii. Hayo ameyabainisha Mkuu wa Wilaya ya Ilala leo Novemba 7, 2023 wakati akizindua mpango wa ugharibishaji wa huduma za chanjo ya magonjwa ya mlipuko katika Ukumbi wa Meya uliopo Arnatoglou Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo amesema "Tumeandaa utaratibu mzuri wa kupambana na adui wa afya kwani mpango huu wa uwezeshaji Jamii kutambua changamoto za kiafya na kuweka mikakati ya kukabiliana na changamoto hizo utafanyika kwa asilimia mia katika tarafa zetu za Segerea na Ukonga hivyo niwashukuru wadau wetu TIP na UNICEF kuwezesha chanjo hii pia niwaahidi tutasimamia kwa ukaribu zaidi zoezi hili na baada ya hapo tutafanya tathmini."
Sambamba na hilo Mhe. Mpogolo ameendelea kusema mpango huu umekua darasa zuri kwa Wilaya ya Ilala kusimamia miradi mingine hivyo kufanya mabadiliko kwenye sekta ya afya huku akihimiza kushirikiana na jamii ili kupata matokeoya chanjo kwa asilimia mia.
Akitoa Shukrani zake wakati wa uzinduzi huo Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam Ndg. Jomaary Satura ameahidi kutekeleza yote yaliyoelekezwa huku akieleza kuwa Halamashauri ya Jiji la Dar es Salaam kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri itaendelea kuboresha huduma za afya na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya na kwa wakati sahihi.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Dkt. Zaituni Hamza ameeleza kuwa “Uzinduzi wa chanjo hii ni mkakati wa kutokomeza magonjwa ya mlipuko hivyo tunaomba kushirikiana na viongozi wetu kuhakikisha mnasimamia Agenda ya Mheshimiwa Rais ya kutokomeza magonjwa ya mlipuko hasa kipindi hichi cha mvua hivyo tuhakikishe wananchi wanapata chanjo ya mlipuko ili kukabiliana na magonjwa ya milipuko pindi yanapotokea."
Naye Afisa Programu sehemu ya elimu ya afya kwa umma kutoka Wizara Afya Bw. Simon Nzilibili ameeleza kuwa afua ya uraghibishaji wa huduma za chanjo kwa viongozi wa kijamii imelenga kuhamasisha matumizi endelevu ya huduma za chanjo kwa watoto chini ya miaka 5 ambao hawajapata chanjo au hawajakamilisha chanjo ndani ya Wilaya ya Ilala walau asilimia 50 hadi Mwezi Desemba, 2023 kupitia mpango wa uwezeshaji jamii kutambua changamoto za kiafya na kuweka mikakati ya kukubaliana na changamoto hizo ambapo kwa Wilaya ya Ilala mpango huo utahusisha mitaa 131 ndani ya Tarafa za Ukonga na Segerea (70 Ukonga, 61 Segerea), WAJA 189 pamoja na wahudumu wa afya 189 huku jumla ya familia 259,200 sawa na asilimia 56.5 ya familia zote 458,614 zilizopo Wilaya ya Ilala zinatarajiwa kufikiwa.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.