Na: Doina Mwambagi
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Edward Mpogolo, amesema Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam itaendelea kufanya kazi na wakandarasi wazawa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ili kukuza uchumi wa ndani na kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa miradi ya Serikali.
Amesema hayo leo tarehe 17 Februari 2026 katika hafla ya makabidhiano ya mradi wa madarasa ya Kidato cha Tano na Sita yenye lift katika shule ya sekondari Bonyokwa , kati ya Mkandarasi Platinum na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, ilofanyika katika shule hiyo.
Akizungumza katika hafla hiyo Mheshimiwa Mpogolo ameonya kuwa Serikali haitawavumilia wakandarasi wazembe watakaokwaza juhudi za maendeleo, huku akisisitiza kuwa itaendelea kuwaamini na kuwapa nafasi wakandarasi wazawa wenye uwezo na wanaotekeleza miradi kwa ubora unaotakiwa.
“Nawataka wakandarasi wajifunze kupitia miradi iliyokamilika na kuzingatia viwango vya ubora vinavyotakiwa. Halmashauri ya Jiji la dar es salaam itaendelea kuwapa kipaumbele wakandarasi wazawa kwa lengo la kuwainua kiuchumi, lakini hatutawavumilia wakandarasi watakaoshindwa kutekeleza majukumu yao kwa wakati au kwa ubora unaokubalika,” amesema Mheshimiwa Mpogolo.
Aidha, Mheshimiwa Mpogolo amesema dhamira ya Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira bora ya ufundishaji na ujifunzaji ili kuboresha sekta ya elimu nchini. Ameeleza kuwa ujenzi wa madarasa ya kisasa yenye miundombinu rafiki ikiwemo lift ni kielelezo cha namna Serikali inavyoendelea kuwekeza katika elimu kwa vitendo.
Pia amewaasa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Bonyokwa kuyatunza madarasa hayo mapya ili yaweze kuwanufaisha wao na vizazi vijavyo, akisisitiza kuwa ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha miundombinu hiyo inalindwa na kutumika ipasavyo kwa manufaa ya taifa
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.