Na: Doina Mwambagi
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mheshimiwa Edward Mpogolo leo Januari 7, 2026 amekutana na Wakuu wa shule za Msingi na Sekondari zilizopo ndani ya Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam kwa lengo la kuweka mikakati ya kuhakikisha msimu mpya wa masomo unaanza kwa ufanisi.
Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa Karimjee, Mhe.Mpogolo amesisitiza umuhimu wa maandalizi ya mapema, usimamizi thabiti wa taaluma na nidhamu, pamoja na uwajibikaji wa wakuu wa shule katika kusimamia mazingira bora ya ufundishaji na ujifunzaji.
Aidha, ameagiza wakuu wote wa Shule kuandaa na kuwasilisha changamoto zinazokabili shule zao zikiwemo changamoto za miundombinu, uhaba wa walimu, vifaa vya kujifunzia na kufundishia, pamoja na masuala ya nidhamu na ustawi wa wanafunzi, ili Serikali ya Wilaya iweze kuweka mikakati ya haraka na ya kudumu ya kuzitatua.
Akizungumza kuhusu uendeshaji wa shule, Mkuu huyo wa Wilaya amesisitiza umuhimu wa mahusiano mazuri ya kikazi kati ya walimu na viongozi wa shule huku akieleza kuwa mahusiano hayo ni msingi wa utekelezaji mzuri wa majukumu ya kila siku na mafanikio ya shule kwa ujumla.
“Ninamtaka kila Mkuu wa Shule ahakikishe kunakuwepo na mawasiliano ya wazi ndani ya shule, kusikiliza changamoto na kuzitafutia ufumbuzi kwa wakati. Migogoro ya kikazi isipotatuliwa mapema huathiri utendaji wa shule na matokeo ya wanafunzi,” Amesema Mhe. Mpogolo.
Kikao hicho ni sehemu ya jitihada za Wilaya ya Ilala katika kuhakikisha shule zote zinafanya kazi kwa ufanisi na kutoa elimu bora kwa wanafunzi katika msimu mpya wa masomo.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.