Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita leo tarehe 20 Februari, 2019 amewasilisha mpango na bajeti ya mwaka 2019/2020 wa jumla ya shilingi bilioni 45.1 ikiwa ni bajeti ya mishahara ya watumishi, matumizi ya kawaida na za utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo.
Mpango na bajeti hiyo umepitishwa kwa kauli moja na wajumbe wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na kutaka kufikiria katika uwekezaji wa miradi mikubwa ili kufanana na majiji mengine duniani yenye ukubwa kama Jiji la Dar es Salaam.
Bajeti ya Halmashauri ya Jiji katika mwaka 2019/2020 imeandaliwa kwa kuzingatia Mwongozo wa bajeti wa mwaka 2019/2020, Dira ya Maendeleo 2025, Malengo endelevu ya Millenia, Sheria ya Bajeti Namba 11 ya Mwaka 2015, Mpango wa maendeleo wa miaka mitano, Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala ya Mwaka 2015 na Maelekezo na Miongozo mingine kama ilivyotolewa na Serikali.
Akizungumzia mpango na bajeti hiyo kwa wakazi na wadau mbalimbali wa Jiji waliohudhuria Mkutano wa Baraza, Meya Mwita amesema kuwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imekadiria kukusanya na kutumia kiasi cha shilingi bilioni 45.1 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo kutoka mbalimbali vya mapato. Kati ya fedha hizo shilingi bilioni 9 zinatarajiwa kukusanywa kutoka kwenye vyanzo vya mapato ya ndani vya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.
Aidha amefafanua kuwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imeendelea kuboresha ukusanyaji mapato yake ya ndani pamoja na kubuni vyanzo vingine vya mapato.
Amefafanua kuwa mpango na bajeti ya mwaka 2019/2020 umelenga kutekelaza mradi wa Kimkakati wa ujenzi wa Kituo Kikuu kipya cha Mabasi cha Mbezi Luis, kuboresha miundombinu ya Dampo, ujenzi wa vyoo vya Umma na kuhakikisha utoaji wa huduma unaoepusha usumbufu kwa jamii.
Amesema Halmashauri pia imepanga kutumia asilimia 60 ya mapato ya ndani sawa na shilingi bilioni 4.7 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na shilingi milioni 797 kwa ajili ya mfuko wa wanawake, vijana na walemavu.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.