Mkuu wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo amewataka wafanyabiashara Kariakoo kuchangamkia fursa katika Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika unaotarajiwa kufanyika Januari 27 na 28 mwaka huu.
Amesema Rais Dk. Samia, amekuwa kinara wa Dunia na Kinara wa Afrika katika matumizi ya nishati safi, hivyo kuanzia Januari 26 Tanzania itaanza kupokea wageni wakiwemo marais kutoka nchi za Afrika ambao watahudhuria mkutano huo.
Mhe. Mpogolo ameyasema hayo leo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, katika Bonza maalumu lililoandaliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) likishirikisha wafanyabiashara wa Mkoa wa kikodi wa Kariakoo.
“Ninawaomba wafanyabiashara kujiandaa kupokea wageni hawa.Mkutano huo utahudhuriwa na marais kutoka nchi nyingi za Afrika ambao watapenda kufika Kariakoo au kutuma wawakilishi wao hivyo ni vyema wafanyabiashara wa Kariakoo kujiandaa kimataifa." ameeleza Mhe. Mpogolo.
Amesema ni wakati wa kuifanya Kariakoo kuwa ya Kimataifa ambapo serikali itatoa mabango maalumu ya mkutano huo.
Aidha, Mhe. Mpogolo amebainisha Soko la Kariakoo ni tegemeo kubwa kwa Wilaya ya Ilala, Mkoa wa Dar es Salaam na taifa kwa ujumla katika ukusanyaji mapato hivyo kuahidi ushirikiano mkubwa kwa wafanyabiashara na Mamlaka ya Mapato.
Aliishukuru TRA kwa ufanisi mkubwa ambapo ufanisi huo umeifanya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kukusanya sh. bilioni 101 katika mwaka wa fedha 2023/24 ambapo malengo ya awali yalikuwa ni kukusanya sh. bilioni 81 tu.
“Kwa kasi hii ya TRA katika ukusanyaji mapato Mwaka huu wa fedha tutajiwekea malengo ya kukusanya hata sh. bilioni 120,” amesema Mhe. Mpogolo.
Ameeleza Serikali wilayani Ilala, itaendelea kushirikiana na TRA na wafanyabiashara wote kwa sababu inatambua umuhimu wa kodi katika maendeleo ya miradi mbalimbali.
“Rais Dk. Samia, alitulietea zaidi ya sh. bilioni 350 za maendeleo Ilala. Tumefanikiwa kutekeleza miradi mingi, ikiwamo ya elimu, afya na barabara." Amebainisha.
Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo, Seveline Mushi, alisema wataendelea kushirikiana na TRA na serikali kwa kulipa kodi kwa wakati.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.