Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Innocent Bashungwa amesema Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imejipanga kumaliza tatizo la foleni katika mkoa wa Dar es salaam kwa kutekeleza miradi ya miundombinu ya barabara na madaraja yenye thamani ya zaidi ya bilioni 222.
Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini wa mkataba wa ujenzi wa daraja la Jangwani leo Oktoba 22, 2024, Waziri Bashungwa amesema nia ya Serikali ni kuhakikisha inamaliza changamoto ya usafiri katika mkoa wa Dar es salaam na katika mikoa mingine hapa Nchini.
Amesema mradi huo wa ujenzi wa Daraja hilo lenye urefu wa mita 390 litakaloanzia Magomeni hadi Jangwani unatarajia kukamilika katika kipindi cha miezi 24 utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 97.1.
"Sehemu ile (Jangwani) imekuwa ni korofi hasa kipindi cha mvua kumekuwa na foleni kubwa lakini sasa niwaambieni tu wakazi wa mkoa huu na wananchi wote kuwa hii sasa itabaki kuwa historia". Alisema
Mbali na Mradi huo, Waziri huyo wa Ujenzi amebainisha kuwa Serikali imetenga kiasi cha Shilingi bilioni 125 zitakazowezesha kukamilisha miradi mbalimbali ya miundo mbinu ya barabara na madaraja.
Baadhi ya maeneo yatakayonufaika na kiasi hicho cha fedha ni pamoja na mradi wa ujenzi wa daraja la Mzinga Wilayani Temeke, daraja la Kigogo lenye urefu wa mita 50,daraja la mikadi Kigamboni,daraja la Kisarawe na mengine.
Awali akimkaribisha Waziri wa Ujenzi, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Albert Chalamila alieleza faida mbalimbali zikiwemo za kiuchumi zitakazopatika a mara baada ya ujenzi wa miundombinu hiyo itakapokamilika.
Mradi wa ujenzi huo wa daraja la Jangwani unaotekelezwa na kampuni ya CCCC kutoka nchini China utakapokamilika utakuwa ni muarobaini wa foleni na mafuriko katika eneo hilo iliyodumu kwa miaka mingi.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.