Na Doina Mwambagi
Afisa Tarafa ya Ukonga, Bw. Kheri William, amewataka wanafunzi wa Shule ya Sekondari Ukonga kuhakikisha wanapanda miti ya matunda isiyopungua mitatu katika makazi yao ili kuimarisha lishe bora na afya zao kwa ujumla.
Bw. Kheri ametoa wito huo leo tarehe 3 Februari, alipokuwa akizungumza na wanafunzi wa shule hiyo katika kongamano la lishe kwa wanafunzi lililofanyika shuleni hapo, lenye lengo la kuwajengea uelewa kuhusu umuhimu wa lishe bora kwa maendeleo ya afya na taaluma.
Akizungumza katika kongamano hilo, Bw. Kheri amesema kauli mbiu ya “Lishe Bora, Afya Bora kwa Ustawi wa Taaluma ya Wanafunzi” inapaswa kuwa dira ya maisha ya kila siku kwa wanafunzi, akisisitiza kuwa lishe bora ina mchango mkubwa katika kuimarisha afya, kuongeza umakini darasani na kuboresha ufaulu wa wanafunzi.
Aidha, ameongeza kuwa “upandaji wa miti ya matunda utasaidia kupatikana kwa matunda kwa urahisi majumbani, hivyo kuchangia upatikanaji wa virutubisho muhimu kwa wanafunzi na familia zao pamoja na kupunguza gharama za ununuzi wa matunda,” amesema Bw. Kheri.
Kwa upande wake, Kaimu Mratibu wa Lishe wa Jiji la Dar es Salaam, Bi. Neema Mwakasege, amesema matokeo ya tathmini ya hali ya lishe kwa wanafunzi 461 waliopimwa yanaonesha kuwa wanafunzi 428 wana hali nzuri ya lishe, wanafunzi 31 wana utapiamlo wa wastani, huku wanafunzi wawili wakibainika kuwa na utapiamlo mkali.
Bi. Mwakasege amesema takwimu hizo zinaonesha bado kuna haja ya kuendelea kuimarisha juhudi za pamoja katika kuboresha lishe kwa wanafunzi, akisisitiza ushirikiano wa karibu kati ya wazazi na walimu ili kuhakikisha wanafunzi wanapata chakula cha mchana shuleni, hatua itakayosaidia kuboresha afya na uwezo wa wanafunzi katika masomo.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.