Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar imeipongeza Halmashauri ya Jiji la DSM kwa usimamizi thabiti wa fedha zinazotolewa kupitia mpango wa kunusuru kaya masikini unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Nchini TASAF.
Pongezi hizo zimetolewa leo Aprili 16, 2024 wakati wa ziara ya Kamati hiyo ya kukagua mradi wa kivuko cha watembea kwa miguu kilichopo Mtaa wa Kimwani, Kata ya Zingiziwa, kilichojengwa na wanufaika wa TASAF kupitia ajira ya muda kwa walengwa kwa gharama ya Shilingi Milioni 35.2.
Akiongea wakati wa ukaguzi, Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mhe. Mwanaasha Khamis Juma amesema kuwa fedha wanazopatiwa wanufaika wanapaswa kuzitumia kwa ajili ya kuboresha maisha yao na kusonga mbele ili maisha yao yawe tofauti na wakati ambapo walikuwa hawajaanza kupata fedha hizo.
Amesema kuwa Serikali kupitia TASAF ,imedhamiria kuondoa umasikini wa kipato unaowakabili wananchi wengi Nchini na kwamba ili kuunga mkono jitihada za Serikali wananchi ambao ni wanufaika wa mpango huo wanapaswa kutumia fedha hizo kwa kilie kilichokusudiwa.
"Kwanza Niwapongeze kwa kujenga kivuko hiki kwani Mradi huu utatatua kero iliyokua ikisumbua kwa muda mrefu ya kushindwa kuvuka hasa kipindi cha mvua. Hii inaonesha ni jinsi gani kuna usimamizi mzuri wa fedha. Lakini niwaase wanufaika, ni vyema mkakitumia kiasi cha fedha mnachopata kwa malengo mazuri mliyojiwekea, haipendezi kuona mtu umepewa pesa ili umpeleke mtoto wako shule lakini hufanyi hivyo na badala yake unaenda kubadilisha matumizi." Amesema Mhe. Mwanaasha Juma.
Aidha, ameongeza kuwa ukaguzi wa mara kwa mara utakua unafanyika ili kujiridhisha mwenendo wa wanufaika hao.
Kwa upande wake mmoja wa wanufaika wa TASAF kutoka Kata ya Zingiziwa amesema kuwa fedha hizo zimesaidia kupata uhakika wa kupata milo mitatu na kufanya shughuli nyingine za kujipatia kipato pamoja na kuwa na uwezo wa kusomesha watoto.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.