Na: Hashim Jumbe
Kamati ya Fedha na Utawala, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, leo tarehe 27 Septemba, 2021 imefanya ziara ya ukaguzi wa vyanzo vipya vya mapato walivyorithi kutoka kwa iliyokuwa Halmashauri ya Jiji lililovunjwa.
Kamati hiyo iliyoongozwa na Mwenyekiti, Mhe. Saady Khimji kwa niaba ya Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ilianza kwa kukagua eneo la uwekezaji liliopo Barabara ya Barack Obama ambalo limepangishwa kwa kuwekewa Makontena Mawili ya biashara, maeneo mengine yaliyotembelewa ni Ukumbi wa Mikutano wa Karimjee, Kituo cha Radio ya Jiji (City fm) Sehemu ya kupangishia kwa ajili ya mgahawa uliopo jengo la Mkurugenzi wa Jiji, eneo la maegesho ya magari na Ushirika wa Kariakoo 'DDC'
Itakumbukwa kuwa aliyekuwa Rais wa Tano (5) wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt. John Magufuli, tarehe 24 Februari, 2021 kwa mamlaka aliyokuwa nayo chini ya kifungu cha 5(1) cha Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji) Sura ya 288 aliivunja Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na kuipandisha hadhi Halmashauri ya Manispaa ya Ilala kuwa Halmashauri ya Jiji, hivyo mgawanyo wa mali (assets) wa Halmashauri hiyo ulifanyika kwa kuzingatia mahali (Halmashauri) ambapo mali hiyo ilipo.
Akiwa kwenye ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati Mhe. Khimji alielekeza Halmashauri kupitia upya mkataba wa upangishaji wa Kontena 2 zilizopo Barabara ya Barack Obama pamoja na vyoo vya umma vilivyopo eneo hilo
Aidha, Mhe. Khimji alipongeza uwekezaji wa kituo cha radio cha Jiji (City fm) lakini pia aliomba Halmashauri kubeba changamoto zilizopo kwenye kituo hicho na kukifanyia maboresho ili kiendane na hadhi ya Jiji
Mwisho, Kamati hiyo iliahidi ushirikiano na Ushirika wa Kariakoo DCC kwa kuwa ushirika huo kwa sasa upo chini ya Halmashauri
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.