Kamati ya Kudhibiti UKIMWI ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, leo tarehe 26 Oktoba, 2023 wamefanya ziara ya kutembelea na kukagua shughuli zinazofanywa na Taasisi ya Fahari Tuamke Maendeleo iliyopo Kata ya Gongolamboto Mtaa wa Ulongoni yenye lengo la kuhamasisha jamii kwa kusaidia na kuwajengea uwezo watoto, wanawake na vijana waishio katika mazingira magumu pamoja na watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI (WAVIU) ili waweze kukabiliana na changamoto mbalimbali za kimaisha.
Akiongea wakati wa ziara hiyo kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudhibiti UKIMWI Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Mjumbe wa Kamati hiyo Mhe. Lucy Lugome amesema “Nipende kuwashukuru sana Taasisi ya Fahari kwa kazi nzuri mnayoifanya ya kusaidia jamii ya watu wa makundi maalumu hadi kutupelekea Leo hii kuja kukagua miradi yenu japo ni sehemu ya majukumu yetu lakini pia kutambua mchango wenu kama Taasisi katika kutoa Elimu kwa Umma juu ya kudhibiti maambukizi mapya ya VVU na UKIMWI hivyo ziara hii ni sehemu ya utekelezaji wa miradi pamoja na kuhakikisha huduma zote zinazotolewa kwa WAVIU zinatekelezwa katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa Fedha 2023/2024 ulioanza Julai hadi Septemba 2023."
Aidha Mhe. Lugome ameendelea kusema “Ziara yetu imekua na mafanikio zaidi kwani tumeweza kujifunza shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na Taasisi ya Fahari ambayo imekua na mchango mkubwa wa kutoa lishe kwa WAVIU kwa lengo la kuimarisha Afya zao lakini pia mbali na kufanya shughuli hizo kwa weledi napende kutoa wito kuhakikisha wanatafuta Mtaalamu Afya atakaeweza kuwaelekeza watu hao namna gani ya kutumia dawa kama inavyoelekezwa.”
Sambamba na hilo Mhe. Lugome ametoa wito kwa Asasi nyingine pamoja na wadau wengine kuiga mfano wa Taasisi ya Fahari Tuamke Maendeleo huku akiwataka Maafisa wa Ustawi kutoka Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kushirikiana na Shirika hilo ili kuweza kupunguza changamoto za watoto wanaoishi katika mazingira magumu ndani ya Jiji la Dar es Salaam.
Awali akisoma taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Shirika kwa kipindi cha Mwaka 2019-2023 Mkurugenzi wa Shirika hilo Bi. Neema Mchau ameeleza kuwa Shirika la Fahari tuamke maendeleo ni Asasi iliyoanzishwa na kusajiliwa mwaka 2016 chiniya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wanawake na makundi Maalumu ikiwa na lengo la kuanzisha jamii yenye maisha bora na ustawi kupitia ujasiriamali, haki za watoto, hifadhi za mazingira pamoja na uwezeshaji wananchi Kiuchumi, kijamii na kiutamaduni.
Sambamba na hilo Bi. Mchau ameeleza kuwa "Shirika la Fahari Tuamke Maendeleo linajishughulisha na kutoa elimu juu ya umuhimu wa matumizi sahihi ya dawa pamona na kuwapa vyakula na lishe watu waishio na maambukizi ya virusi vya Ukimwi (WAVIU) ambapo hadi kufikia sasa tumeweza kuwafikia WAVIU 20 walioko Kata ya Majohe pia tumekua tukihamasisha utunzaji na uhifadhi wa mazingira kwa kushirikiana na jamii katika kupanda miti ya matunda na vivuli kwenye Taasisi za Serikali ikiwemo Shule za Msingi Bangulo na Ushindi pamoja na Zahanati ya Yongwe na Kituo cha Afya Chanika hivyo nipende kutoa Shukrani zangu kwa wajumbe wote kwa kututembelea leo naahidi ushirikiano naninyi katika kuhakikisha tunatatua changamoto zote zinazohusiana na watoto wa mazingira magumu pamoja na WAVIU wote kwa ustawi wa Jiji letu na Nchi kwa ujumla."
Aidha Kamati imeagiza wataalamu wa afya kuwajengea uwezo Fahari Tuamke Maendeleo wakati wanapotoa huduma kwa WAVIU pamoja na kuwaeleza namna ya kuwa na usiri wakati wanapofanya shughuli za kuhudumia makundi maalumu huku wakiwataka wataalamu hao kufuatilia takwimu za Waviu kwa Fahari Tuamke Maendeleo ili kujua kama wanapatikana kwenye Konga ni wapya.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.