Wananchi wa DSM wamehimizwa kutumia nishati safi ili kutunza mazingira, Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Albert Chalamila aliposhiriki Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani Leo tarehe 5 Juni, 2024 Ambayo kimkoa yamefanyika katika Viwanja vya Mji Mwema Wilayani Kigamboni, Maadhimisho hayo yana kaulimbiu isemayo “Urejeshwaji wa Ardhi, ustahimilivu wa hali ya jangwa na ukame”
Akiongea na viongozi na wananchi waliojitokeza katika Maadhimisho hayo Mhe Chalamila amesema “ Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekua mstari wa mbele kusisitiza matumizi ya nishati safi lengo ikiwa ni kutunza mazingira kwa kutokata miti hovyo, na kuepukana na magonjwa yatokanoya na utumiaji wa nishati isiyo salama. Hivyo nitoe Rai kwenu wananchi kuhakikisha tunatumia nishati safi na tunaungana kwa pamoja kuhakikisha tunaachana na ukataji wa miti kwa ajili ya uchomaji wa mkaa ili kutunza mazingira yetu”
Pia, Mhe. Chalamila amesema Ofisi ya Mkuu wa Mkoa itatoa mitungi ya gesi kwa wanawake mia tatu (300) kwa kila Wilaya ikiwa ni kuunga juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kujali afya zetu kwa maslahi mapana ya maendeleo endelevu ya Taifa letu
Sambamba na hilo, Mhe. Chalamila amewataka Wakuu wa Wilaya zote za Dar es Salaam kwa kushirikiana na Taasisi za mazingira kuhakikisha wanawachukulia hatua za kisheria wale wote wanaofungulia maji machafu katika mikondo ya maji safi, pia amewataka wananchi kuacha tabia ya kutupa taka hovyo ili kujilinda na magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu.
Awali akimkaribisha Mgeni rasmi, Katibu Tawala wa Mkoa wa DSM Dkt. Toba Nguvila amempongeza Mkuu wa Mkoa kwa kukubali kushiriki maadhimisho ya siku ya mazingira Duniani na kuwataka wananchi kutotupa taka ngumu mitaani
“Kumekua na tabia ya wananchi kutupa taka ngumu katika mazingira yetu hivyo tuhakikishe tunakusanya hizo taka kwani ni malighafi kwaajili ya matumizi ya Urejeshwaji yaani kutengeneza bidhaa zingine.“ amesema Dkt. Nguvila.
Siku ya Mazingira Duniani ilianzishwa mwaka 1972 na huadhimishwa kila ifikapo tarehe 5 Juni ya kila Mwaka lengo likiwa ni kutatua changamoto zote zitokanazo na mazingira.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.