“Kwa Maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Chagua Viongozi Bora 2020,” hiyo ni kauli mbiu iliyotumika katika sherehe za wakulima, wavuvi na wafugaji yaliyofanyika katika kanda mbalimbali nchini kuanzia Agosti 1-8, mwaka huu ambao ifikapo mwezi Oktoba Watanzania watatumia haki yao kupiga kura, kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania, kumchangua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wabunge na Madiwani.
Ujumbe huo, bila shaka yoyote, umetumika kuwakumbusha na kuwahamasisha wananchi kutambua kwamba hatma ya mafanikio ya Taifa la Tanzania katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi yapo mikononi mwa wananchi, hivyo wanapaswa kujitokeza na kuwachangua viongozi bora wataoshirikiana nao kuimarisha sekta hizo katika kipindi cha miaka mitano ijayo ya Serikali ya Awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kupitia michango yake mbalimbali katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam nayo ilishiriki kikamilifu katika sherehe hizo maarufu kama Nane Nane ambazo katika Kanda ya Mashariki zilifanyika katika viwanja vya Julius Kambarage Nyerere mjini Morogoro zikihusisha mikoa ya Tanga, Pwani, Morogoro na Dar es Salaam.
Kwa kutumia “shamba darasa” wananchi walifundishwa kilimo cha mjini na namna ya kusia, kupanda na kukuza mimea ya mazao ya aina mbalimbali katika maeneo ya mijini. Aidha, Halmashauri ya Jiji iliwaonesha pia wananchi baadhi ya kazi zinazotokana na mazao ya kilimo, uvuvi na ufugaji inazofanywa na wajasiriamali wanaonufaika na mikipo ya asilimia 10 inayotokana na mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.
Katika maonesho hayo ya Nane Nane, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam pia ilionesha mchango mkubwa unaotolewa na Shirika la Masoko Kariakoo, Shirika la Maendeleo na Uchumi Dar es Salaam (DDC) na Dar es Salaam City Council Business Park ambayo wengi huitambua kwa jina la Machinga Complex.
“Nimefurahishwa sana na maonesho yenu Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na endeleeni kuwajengea uwezo hao wajasiriamali kwa kuwapatia hiyo mikopo, mmejiaandaa vizuri”, alisema Mheshimiwa Jumaa Aweso, Naibu Waziri wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji ambaye alitembelea maonesho ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.