Katika jitihada zinazoonekana kuwa na mafanikio makubwa katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, Jiji la Dar es Salaam kwa kushirikiana na Umoja wa Majiji Duniani, C40 Cities, linatarajia kuanza rasmi utekelezaji wa mpango wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika Jiji la Dar es Salaam ulioandaliwa na Mamlala za Serikali za Mitaa katika Jiji la Dar es Salaam kwa kushirikiana na C40 Cities na wadau mbalimbali.
Akifungua warsha ya siku mbili ya wataalam katika sekta ya mabadiliko ya tabianchi iliyoanza Disemba 1, 2022 katika Ukumbi wa Mikutano wa hoteli ya Holiday Inn jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam Joshua Muhogolo amesema kuwa mpango huo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika Jiji la Dar es Salaam.
Muhogolo amewataka washiriki wa warsha hiyo kutumia fursa hiyo kuongeza ujuzi wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa manufaa ya umma.
"Nimejulishwa kwamba C40 Cities itaendelea kutoa mafunzo zaidi kupitia warsha kama hii, ninawataka mtumie fursa hizi kwa manufaa ya umma kwa kufanikisha malengo ya Serikali katika Jiji la Dar es Salaam dhidi ya mabadiliko ya tabianchi" alisema Muhogolo.
Kwa upande wake mwakilishi wa C40 Cities ambaye ni mshauri wa masuala ya mabadiliko ya tabianchi, Jophillen Bejumula, ametoa wito kwa washiriki wa warsha hiyo kuunganisha nguvu ili kufanikisha utekelezaji wa mpango huo ambao utasaidia kutatua changamoto zinazosababishwa na mabadiliko ya tabianchi na kuzuia athari zaidi zinazoweza kusababishwa na mabadiliko ya tabianchi.
Warsha hiyo iliyoandaliwa na C40 Cities imewaleta pamoja wataalam kutoka katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Manispaa ya Ubungo, Kinondoni, Kigamboni na Temeke kutoka katika sekta ya udhibiti taka, fedha, mipango, ardhi, maendeleo ya jamii, kilimo na ushirika, biashara viwanda na uwekezaji.
C40 Cities ambayo ni umoja wa zaidi ya majiji 97 Duniani imekuwa ikishirikiana na Halmashauri ya Jiji za Dar es Salaam kwa zaidi ya miaka saba katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ikiwajengea uwezo wataalam wa Dar es Salaam kwa kuwapatia mafunzo ndani na nje ya nchi ili kufanikisha adhma ya Serikali katika Jiji la Dar es Salaam ya kupambana na janga la mabadiliko ya tabianchi
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.