Wazazi na Walezi wametakiwa kuhakikisha watoto wanapata mlo kamili wenye virutubisho vyote muhimu vya makundi ya chakula kwa ajili ya ukuaji wa binadam ikiwemo protini, wanga, vitamini, madini, mboga mboga, matunda na maji.
Hayo yamebainishwa leo tarehe 29 Machi, 2023 na Afisa Lishe Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Bi. Neema Mwakasege wakati wa zoezi la utoaji wa Elimu kwa vitendo juu ya masuala ya lishe, lililoendeshwa katika Kata ya Mnyamani ambapo amewasisitiza wazazi na walezi kuhakikisha watoto hawakosi mlo wenye makundi yote ya chakula ili kuwakinga na maradhi sambamba na kuwakinga dhidi ya udumavu.
"Wapeni watoto chakula chenye mjumuisho wa makundi yote muhimu katika kila mlo, Maji hayamo katika makundi hayo lakini msiache kuwapa maana maji ndio sehemu kubwa katika mwili wa binadamu na ndio yanayosaidia makundi yote hayo yaweze kufanya kazi kwa urahisi mwilini. Vilevile nisisitize kula mbogamboga kwa wingi kwani husaidia kuongeza damu mwilini." Alisema Bi. Mwakasege.
Nae Bi. Sophia Elias, Afisa Ustawi wa Jamii kutoka Kituo cha Afya Buguruni amewaomba wazazi na walezi kuacha tabia ya kukatisha kuwapeleka watoto kliniki pindi wanapofikisha miaka miwili na nusu hasa baada ya kumaliza chanjo zilizozoeleka ikiwemo ile ya ugonjwa wa Surua, mlango wa kizazi, kupooza, homa ya Uti wa Mgongo na ile ya kujikinga dhidi ya ugonjwa wa kifua kikuu.
Aidha, Afisa Mtendaji wa Kata ya Mnyamani Ndg. Javari Mrisho alilisitiza suala la Ukatili wa Kijinsia unaofanyika majumbani na kuwaasa wananchi kutoa taarifa haraka pindi wapatapo taarifa za matukio hayo.
"Wananchi msiwe waoga kutoa taarifa. Watu wanafanyiwa ukatili lakini kwa uoga hawatoi taarifa kwenye vyombo husika. Nawaasa nikiwa kama Mtendaji wa Kata kama ni wewe unafanyiwa ukatili au una taarifa za mtu yoyote anaefanya au kufanyiwa ukatili wa kijinsia basi utoe taarifa mara moja." Amesema Ndg. Mrisho
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.