Wajumbe wa Kamati ya Huduma za Jamii wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Bi. Leyla Hussein Madibi, Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita Charles pamoja na Waheshimiwa Madiwani na Wajumbe wa Kamati hiyo wamefanya ziara ya kuvitembelea vikundi vya kina mama na vijana vinavyonufaika na mikopo inayotolewa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa vikundi hivyo.
Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam katika kutekeleza agizo la Serikali la kutenga asilimia kumi (10%) ya mapato yake ya ndani ili zitumike kwa ajili ya mfuko wa kukopesha wanawake na vijana ili wajikwamue kiuchumi, kujiongeza kipato na kupunguza tatizo la ajira hasa kwa vijana na kina mama ilitenga fedha na kuvikopesha vikundi kumi na nane (18).
Vikundi hivi vinajihusisha na miradi ya uuzaji wa nafaka, utengenezaji wa samani za ndani, ufugaji wa kuku, mama lishe, uuzaji wa vocha, utengenezaji wa mikoba ya mikutano, sendozi za kina mama, pochi za wanawake kwa kutumia ukili, umaliziaji wa vibanda vidogo vidogo vya biashara, uzoaji wa taka katika makazi ya watu, upambaji na upishi, vicoba, ushonaji, uuzaji sabuni ya maji pamoja na utengenezaji wa juisi.
Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam inavikaribisha vikundi zaidi vya kina mama na vijana ili viweze kunufaika na fursa za mafunzo ya ujasiriamali pamoja na mikopo ili wajikwamue kiuchumi, kujiongeza kipato na kupunguza tatizo la ajira hasa kwa vijana na kina mama.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.