Na Neema Njau
Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imeendelea kutekeleza kwa Madhubuti agizo la Serikali ya Awamu ya sita inayoongozwa na Mhe Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania la Halmashauri zote nchini kutenga 10% ya mapato yake ya ndani kuwezesha wanawake, vijana na watu wenye Ulemevu.
Katika banda la Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwenye maonesho ya nane nane Kanda ya Mashariki 2022 yanayofanyika mkoani Morogoro, yanayohusisha mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga, na Morogoro yenye kauli mbiu “ Agenda 10/30 : Kilimo ni Biashara, Shiriki kuhesabiwa kwa Mipango bora ya Kilimo, Mifugo, na Uvuvi “ Halmashauri imeweza kushirikisha vikundi mbalimbali vya wadau wa Kilimo, mifugo na uvuvi ambavyo vimewezeshwa kwa mkopo wa 10% ya mapato yake ya ndani ambavyo vimeweza kuongeza ubora katika uzalishaji pamoja na thamani ya bidhaa zao na kuweza kukuza uchumi wao.
Tatu Seleman ni mjasiriamali kutoka kikundi cha Gogolika ambacho kina wanachama saba “7”, awamu ya kwanza walipewa sh milioni tatu na sasa wameomba tena awamu ya tatu.
Tatu anasema wao ni wanufaika wakubwa katika mkopo huo wa Halmashauri kwa kuwa awamu ya kwanza waliweza kununua mashine za karanga, vifungashio na Brenda hapo ilikuwa ni mwaka juzi.
“Mkopo wa pili tumepata sh milioni 10 mwaka jana, ulituwezesha kupata ofisi, lakini kuna wajane walinufaika kusomesha watoto wao, kuna vikundi vya vijana tumewaanzishia wamepata usajili na sasa wanazalisha pilipili, tayari wana mashine,” anasema.
Mbali na hayo anasema pia wameweza kupata mafunzo ya kilimo cha mjini cha mboga mboga.
Anasema hivi sasa mkopo wa tatu bado wanaufuatilia na tayari wameshafanya usajili kupitia mtandao.
Akielezea faida walizopata anasema ni nyingi kwa kuwa kila mwanakikundi sasa ana uwezo wa kujitegemea na amesimama mwenyewe.
“Faida nyingine tumepata elimu na mafunzo ya SIDO ya usindikaji, pamoja na jinsi ya kutafuta masoko,” anasema.
Anaeleza kuwa wanatengeneza vitunguu saumu, viungo vya chai, viungo vya mchuzi, pilau na mafuta ya nazi.
Changamoto iliyopo ni kwamba kwenye soko uelewa wajamii ni mdogo kwa kuwa hawajakubali bidhaa za watanzania wenzao.
Mjasiriamali mwingine ni Avitus Mkonge kutoka kikundi cha ‘Long Life One’ kilichopo Kitunda Jijini Dar es Salam, anasema kikundi hicho wapo watano wanajihusisha na usindikaji wa vyakula asilia vya lishe na viungo vya pilau.
Mkonge anasema mkopo wa kwanza walipata sh milioni 200 ambazo walizalisha bidhaa hizo walizozieleza na kwamba soko lao lipo Tanzania nzima.
“Upande wa lishe tuna aina nne tofauti ambazo tunachanganya nafaka tofauti tofauti zinazosaidia tiba lishe na kujenga afya,” anasema.
Anasema katika michanganyiko yao wanatumia mbegu za chia, maziwa ya soya, mbegu za maboga, mbegu za mchicha, almondi, ufuta, mahindi lishe, soya lishe na karanga kutokana na aina ya lishe wanayoitaka.
Naye Mjasiriamali wa usindikaji kutoka kikundi cha Upendo, Emmanuel Msinga anaelezea teknolojia walizonazo ambazo waliwezeshwa na Halmashauri hiyo kuwa ni mashine za kuchakata mihogo, kukuna nazi, kusaga karanga, kutengeneza juisi pamoja na teknolojia ya kukaushi matunda na mboga mboga.
Anasema wamekuwa wakichakata mazao ili kuzuia upotevu wake kwani kipindi cha mavuno ya mihogo mingi hupotea hivyo huichakata na kutengeneza bidhaa mbalimbali.
“Pia tuna teknolojia ya kukaushia matunda, msimu wa matunda mengi. Kutokana na teknolojia tuliyonayo tuna uwezo wa kuuza maembe msimu yote na nanasi, pamoja na fenesi,” anasema.
Anasema kwenye uchakataji huo wa matunda wameweza kupata soko nchini Marekani pamoja na Geneva.
Anasema katika soko la Marekani sasa wana miaka miwili lakini wanahitaji mzigo mkubwa ambao wao hawakidhi.
“Mwaka jana tulipewa oda ya tani 2.5 tukasafirisha tan 1.6 za nanasi, embe na fenesi. Mwaka huu tumepata oda ya tani mbili mpaka sasa tumepeleka kilo 800,” anasema.
Anasema kinachowakwamisha ni vifaa vya kisasa vya kukaushia.
Katika hatua nyingine anasema Halmashauri hiyo imewawezesha mkopo wa sh milioni 18 mwaka jana kwa ajili ya kilimo cha mboga mboga , migomba na papai katika eneo la Chanika.
“Faida tuliyoipata tumenunua ng’ombe wanne, watatu wamezaa tunasambaza mazinwa na kupeleka viwandani, wanazalisha lita 40 kwa siku na lita moja rejareja sh 2000 kwa ujumla sh 1500,” anasema.
Mkuu wa Idara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi katika Halmashauri hiyo, Majaliwa Andrea anasema fursa zipo za uzalishaji, soko la bidhaa lipo ni suala tu la wananchi kutumia fursa zilizopo kuhakikisha mazao yanayozalishwa yanachakatwa na kuuzwa kwa lengo la kujipatia kipato kwa watu binafsi na kuwezesha serikali kukusanya mapato ambayo ni chanzo cha maendeleo ya nchi katika sekta mbalimbali za elimu, afya,miundombinu ya barabara Pamoja na kutenga 10% ya mapato ya ndani ambayo ni mikopo kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Anataka wananchi kutumia fursa zilizopo katika ardhi iliyopo.
Naye Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii katika Halmashauri hiyo, Francisca Makoye anasema ushiriki wao katika maonyesho hayo ni kuonyesha jitihada za serikali kupitia asilimia 10 ya mapato ya ndani ambayo yamelenga kuwezesha wanawake, vijana na wenye ulemavu kiuchumi.
“Shughuli za wajasiriamali tuliokuja nao zinaenda sambamba na ajenda ya mwaka huu kupitia mikopo. Wanawake wajasiriamali kuboresha biashara na bidhaa zinazotokana na kilimo, mifugo na uvuvi ili kuendeleza mnyororo wa thamani,” anasema.
Anatoa mfano kuwa Halmashauri hiyo imewezesha vikundi vya vijana vinavyojishughulisha na usindikaji na uzalishaji wa vyakula lishe, kwa upande wa wanawake wamewezesha viwanda vidogo vinavyozalisha viungo mbalimbali vya kula.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.