Na: Shalua Mpanda
Mikataba 6 yenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 4 imevunjwa katika kipindi cha miezi mitano katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kufuatia baadhi ya wakandarasi kutotimiza masharti ya mikataba yao.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Jiji hili Elihuruma Mabelya wakati wa hafla fupi ya kusaini mkataba wa pili na mkandarasi kampuni ya KIKA Construction Company Ltd wa ujenzi wa shule ya sekondari Kipunguni.
Mkurugenzi huyo amesema lengo la Serikali ni kuona miradi ya maendeleo inakamilika kwa wakati hivyo hawatasita kuvunja mikataba kwa wakandarasi ambao hawatatimiza masharti ya mikataba yao na kuwataka kufanya kazi usiku na mchana.
"Mradi huu wa ujenzi wa shule ya Sekondari Kipunguni ni moja ya miradi ambayo ilisimama kwa muda mrefu na watoto wetu walikuwa wanapata shida kufuata elimu mbali na hapa". Alisema Mabelya
Akiongea na wananchi katika hafla hiyo,Mbunge wa Jimbo la Ukonga Mheshimiwa Jerry Slaa amesema kata hiyo ya Kipunguni haikuwa na shule ya Sekondari hivyo anamshukuru Mhe.Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuleta fedha za ujenzi huo.
Mkataba huo uliosaniwa leo unamtaka Mkandarasi huyo kukamilisha umaliziaji wa jengo hilo la ghorofa lenye vyumba 20 na vyoo 45 ndani ya miezi sita.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.