Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Aboubakar Kunenge amesema ifikapo Alhamisi ya Februari 25, 2021 Kituo kipya cha kimataifa cha mabasi yaendayo mikoani na nje ya nchi cha kilichopo eneo la Mbezi Luis jijini Dar es Salaam kitaanza rasmi kutoa huduma na Kituo mabasi Ubungo kilichokuwa kikitumika awali hakitotumika tena.
RC Kunenge amesema wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam ambapo hatua hiyo imekuja baada ya kukamilika kwa miundombinu yote muhimu ikiwemo majengo, maegesho, barabara na ofisi za kutoa huduma katika Kituo hicho.
“Kituo hiki kimekamilika kabisa kipo tayari kwa kutumika, hivyo tunawataka Watanzania kuanza kutumia kituo hicho na tunatarajia kuanza kutumika rasmi siku ya Alhamisi” Amesema Kunenge.
Kunenge amesema Serikali imetoa siku tatu kuanzia Jumatatu Februari 22 mwaka huu mpaka Jumatano kwa wanaotoa huduma kuanza kuanza kujiandaa na kujipanga kwa ajili ya matumizi ya Kituo hicho.
Aidha, RC Kunenge amesema tayari Serikali imekutana na wadau wote husika ikiwemo Chama cha Wamiliki wa Mabasi "TABOA" na wote wamejiridhisha kuwa Kituo kimekamilika na kipo katika hali nzuri ya kutoa huduma hivyo wapo tayari kutoa huduma.
Vilevile, Kunenge amewataka wasafiri watakaotumia kituo hicho kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya ugonjwa COVID-19 kama taarifa ilivyotolewa na Serikali.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Bi. Sipora Liana, amesema ifikapo siku ya Jumanne watafanya kikao na watoa huduma wote watakaokuwa wakitoa huduma ndani ya jengo na siku ya Jumatano watakutana na Wamachinga, baba na mama lishe kwa ajili ya kuwekeana mikakati ya biashara.
Liana amesema lengo la kukutana na watoa huduma hao ni kuweka utaratibu mzuri wa kufanya kazi katika Kituo hicho cha mabasi cha Kimataifa.
Naye Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam Lazaro Mambosasa amesema Jeshi la Polisi limejipanga kuhakikisha abiria wote wanaosafiri au kuingia kituoni hapo hawapati usumbufu wa aina yoyote.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.