Historia imeandikwa nchini Tanzania tarehe 27 Machi, 2017 mara baada ya Serikali kuzindua rasmi tovuti za Mikoa yote 26 ya Tanzania Bara na Mamlaka za Serikali za Mitaa 185. Hafla ya uzinduzi huo ulifanywa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. George Simbachawene (Mb), na kuhudhuriwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (Mb), na Mkurugenzi Msaidizi wa USAID Tanzania, Tim Donnay, ambao ndio wafadhili wa Mradi wa Uimarishaji Mifumo ya Sekta za Umma (PS3).
Waziri Simbachawene katika hotuba yake ameishukuru na kuipongeza Shirika la Msaada la watu wa Marekani, USAID kupitia Mradi wa Uimarishaji Mifumo ya Sekta za Umma “PS3”, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Wakala ya Serikali Mtandao kwa kushirikiana pamoja katika kusanifu mfumo wa pamoja “Government Website Framework” ambao umesaidia kutengeneza na kusimamia tovuti za Serikali zenye kiwango na muonekano mmoja ambao ni rahisi wakati wa kufanya maboresho ya pamoja, rahisi na rafiki kwa mtumiaji pindi watakapokuwa wanazitembelea.
Mhe. Simbachawene ameendelea kufafanua kwamba suala la upatikanaji habari na taarifa mbalimbali ni takwa la kisheria na kikatiba, hivyo basi viongozi wa taasisi za umma wana wajibu wa kuhakikisha kuwa taarifa mbalimbali za utekelezaji Serikalini zinawafikia wananchi kwa usahihi na kwa wakati.
Katika hatua nyingine, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (Mb), ameeleza kuwa tovuti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa ni njia rahisi na bora ya kuwafikishia wananchi taarifa za utekelezaji Serikalini. Amefafanua kwamba, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha sheria mbili zinazowapa wananchi haki ya kupata taarifa na habari.
Mhe. Mwakyembe, amewakumbusha maofisa habari na TEHAMA wajibu wao wa kuzihudumia tovuti na kuhakikisha kuwa taarifa sahihi zinawafikia wananchi kwa uwazi na kwa wakati na pia ametoa wito kwa viongozi wa taasisi za umma kuwapa ushirikiano maofisa habari na TEHAMA wanapohitaji taarifa za kuwekwa kwenye tovuti kwani mafanikio na uhai wa tovuti hizo hayatamtegemea mtu mmoja.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.