Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo, ametoa angalizo kwa Watendaji katika Wilaya hiyo watakaoshindwa kukamilisha miradi kwa wakati na viwango vinavyohitajika kuwajibishwa.
Mhe. Mpogolo ameyasema hayo leo Februari 24, 2024 wakati akifungua mafunzo ya usimamizi wa miradi (project management) yaliyoandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ilala kwa kushirikiana na Taasisi ya Usimamizi wa Miradi (TIPM) yanayofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Arnatoglou.
Mhe. Mpogolo amesema mafunzo hayo ni matokeo ya mwaka mmoja baada ya kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo na kubaini uwepo wa mapungufu ambapo amesema kuwa kupitia mafunzo hayo, Watumishi wa Jiji la DSM watakuwa na uwezo wa kuisimia miradi kikamilifu.
"Mafunzo haya ni matokeo ya mwaka mmoja baada ya kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo na kubaini mapungufu katika miradi hiyo kwa wahandisi, watu wa manunuzi, wachumi n.k hivyo natumai kupitia mafunzo haya miradi itakamilika kwa viwango vinavyohitajika na wakati ikiwa pamoja na utolewaji wa taarifa kwa wakati." Amesema Mhe. Mpogolo.
Aidha ameongeza kuwa, Halmashauri ya Jiji la DSM ndiyo Halmashauri inayoongoza kwa mapato kuliko Halmashauri zote nchini hivyo ni vyema hata miradi yake ikawa yenye viwango huku akiwataka Watendaji wa Kata kutoa taarifa sehemu husika pindi wanapoona kusuasua kwa miradi.
Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam Mhe. Omary Kumbilamoto amemshukuru Mkuu wa Wilaya hiyo kwa kuwapa fursa ya mafunzo hayo ambayo anaamini yataleta Mabadiliko katika miradi mingi ikiwa pamoja na kukamilika kwa wakati.
Nae Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam Jomaary Satura amesema kupitia mafunzo hayo atahakikisha anaongeza nguvu katika Mapinduzi ya usimamizi kamilifu wa miradi inayoendelea na ile ambayo ipo kwenye mipango.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.