Na: Doina Mwambagi
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Edward Mpogolo, amewataka Wenyeviti wa Mitaa, Watendaji wa Mitaa na Kata kuheshimu dhamana waliyopewa kwa kuhakikisha shughuli zote za kiofisi zinafanyika ofisini badala ya nyumbani.
Akizungumza leo na viongozi hao, aliwakumbusha kuwa nafasi walizo nazo ni jukumu kubwa linalopaswa kutekelezwa kwa uadilifu na uwajibikaji.
Aidha, Mhe. Mpogolo aliwataka viongozi hao kutumia mamlaka yao kwa maslahi mapana ya wananchi, akisisitiza kuwa ofisi za Serikali za Mtaa na Kata ndizo ngazi za kwanza za kushughulikia mahitaji ya wananchi.
Aliwakumbusha kuwa huduma bora kwa wananchi huanzia kwa utendaji makini wa viongozi wa ngazi ya chini.
Katika hotuba yake, alisisitiza pia mshikamano na ushirikiano kati ya wenyeviti wa Mitaa na Watendaji wa Mitaa na Kata, akieleza kuwa mafanikio katika utawala wa mitaa yanahitaji kazi ya pamoja. Ushirikiano thabiti utawezesha utekelezaji wa majukumu kwa ufanisi na kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Mbali na hayo, alitoa maagizo ya kuzingatia usafi wa mazingira katika maeneo yao.
Aliwataka viongozi hao kuhakikisha kuwa jamii inahamasishwa kudumisha usafi ili kuimarisha afya na ustawi wa wananchi wa Ilala.
Mkutano huo ulilenga kuwaimarisha viongozi wa ngazi ya mtaa na kata katika utendaji wao wa kila siku, huku Mkuu wa Wilaya akisisitiza kuwa nidhamu na uwajibikaji vitasaidia kuboresha maisha ya wakazi wa Ilala.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.