Na: Doina Mwambagi
Mkurugezni wa Tume Huru ya Uchaguzi Tanzania Ramadan Kailima amesema uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa mkoa wa Dar es salaam utafanyika kwa siku saba pekee na hakutakuwa na siku za nyogeza.
Ameyasema hayo Machi 10 ,2025 wakati wa ziara ya kukagua zoezi la mafunzo ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu kwa waandikishaji wasaidizi ngazi ya Jimbo yaliyofanyika katika ukumbi wa Anartoglo Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi huyo amesema Tume Huru ya Uchaguzi imejipanga kwa kuwa na mashine (BVR) za kutosha za kufanya zoezi hilo katika mkoa wa Dar es salaam hivyo wakazi wa mkoa wa Dar es salaam wanapaswa kujitokeza kwa wingi katika siku hizo zilizotengwa kupata huduma hiyo ya kuboresha taarifa zao.
Amebainisha kuwa zoezi hilo kwa mkoa wa Dar es salaam linatarajiwa kuanza rasmi siku ya Jumatatu Machi 17, 2025 na linatarajiwa kukamilika Machi 23, 2025, hivyo wakazi wa mkoa huu wanapaswa kuzitumia siku hizo saba kuhakiki na kuboresha taarifa zao.
"Uandikishaji utafanyika kwa siku saba tu, hatutaongeza siku, hivyo ni muhimu kwa kila mmoja kujitokeza kwenye vituo vilivyoandaliwa kwenda kuboresha taarifa zake mapema bila kuchelewa." Alisema Kailima.
Awali akizungumza na waandikishaji hao wasaidizi, Mkurugenzi huyo wa Tume amewataka watendaji kuhakikisha wanatambua kata zao vizuri na kuzijua changamoto zilizopo katika maeneo yao.
Uboreshaji wa daftari ni hatua muhimu kuelekea zoezi la Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, hivyo wananchi hasa wakazi wa Jiji la Dar es salaam hawana budi kujitokeza kwa wingi kuhakiki na kuboresha taarifa zao katika muda huo uliopangwa.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.