TIMU ya UMITASHUMTA Wilaya ya Ilala, leo tarehe 30 Mei, 2024 wameibuka Mabingwa wa Jumla wa Mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) ngazi ya Mkoa wa Dar es Salaam, mashindano yaliyofanyika kwa Siku Nne (04) katika viwanja vya Shule ya Sekondari Jitegemee vilivyopo Temeke, Dar es Salaam
Mashindano hayo yaliyoshirikisha Timu Tano (05) kutoka katika Wilaya za Mkoa wa Dar es Salaam ambazo ni Wilaya ya Ilala, Kinondoni, Ubungo, Kigamboni na Temeke yalianza tarehe 27 Mei, 2024 na kutamatika leo tarehe 30 Mei, 2024 ambapo Katibu Tawala Mkoa wa Dar es Salaam Dkt. Toba A. Nguvila ndiye aliyekua Mgeni rasmi huku Timu ya Wilaya ya Ilala wakiibuka washindi wa Jumla kwa kubeba Jumla ya Vikombe Kumi na Mbili (12) ambapo Vikombe Tisa (09) ni vya nafasi ya kwanza, Vikombe Viwili nafasi ya Pili (2) na Kikombe Kimoja (1) Ushindi wa Jumla na Nafasi ya Pili ilienda kwa Timu ya Wilaya ya Kigamboni.
Aidha, mashindano hayo yaliwakutanisha jumla ya wanamichezo 600 walioweka kambi Shule ya Sekondari Jitegemee, ambapo Katibu Tawala Mkoa wa Dar es Salaam, Dkt. Toba Nguvila wakati anafunga mashindano hayo amesema
"Nawapongeza sana kwa kufanikisha mashindano haya nafahamu mwaka 2023 tulishika nafasi ya pili ngazi ya Taifa sasa nendeni mkaupambanie Mkoa wetu, hakikisheni mnatuletea vikombe vingi tena nafasi ya kwanza kitaifa msije mikono mitupu , Dar es Salaam ni Mkoa wenye heshima kubwa."
Pamoja na Timu ya Wilaya ya Ilala kushinda Ubingwa wa Mkoa, lakini pia Wilaya ya Ilala imetoa wachezaji 37 kati ya wachezaji 120 wanaounda timu ya Mkoa wa Dar es Salaam itakayokwenda kushiriki michuano hiyo kwa ngazi ya Kitaifa, mashindano yatakayofanyika Mkoani Tabora kuanzia tarehe 05 Juni, 2024 hadi 15 Juni, 2024.
Itakumbukwa kuwa timu ya Wilaya ya Ilala ndiyo walikuwa Mabingwa watetezi wa michuano hiyo kwa Mkoa wa Dar es Salaam na mwaka huu wameweza kutetea tena ubingwa wao.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.