WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo amempongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa kusimamia ujenzi wa stendi mpya na ya kisasa ya Mbezi Luis ambapo ujenzi wake umekamilika kwa kiasi kikubwa
Akiongea na watendaji wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam katika ukumbi wa Karimjee leo tarehe 28 Desemba, 2020 Waziri Jafo amesema, ujenzi wa stendi hiyo hadi sasa umekamilika kikamilifu na kinachosubiriwa ni utoaji wa huduma za usafiri na nyinginezo ili magari yaweze kupita kwa urahisi na ufanisi zaidi.
Aidha Waziri Jafo amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Bi. Sipora Jonathan Liana na watendaji wake kushirikiana na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROAD) kumalizia hatua iliyobakia haraka, ili wananchi waweze kufaidi matunda makubwa kutokana na fedha zilizozitolewa na Mheshimiwa Rais zaidi ya shilingi bilioni hamsini (50) kwa ajili ya mradi huo wa kimkakati.
Katika hatua nyingine Jafo alisema, "Baada ya ujenzi wa Kituo kikuu cha mabasi cha Mbezi Luis kukamilika, stendi ya Ubungo ifungwe haraka sana’’. Hata hivyo Jafo amewasihi watendaji wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kuendelea kuchapa kazi ili Jiji liendelee kufanya vizuri zaidi.
Kituo kikuu kipya cha mabasi kilichopo eneo la Mbezi Luis jijini Dar es Salaam ni miongoni mwa mradi wa kimkakati unaosimamiwa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, ikiwa ujenzi wake umetokana na fedha za ndani chini ya uongozi wa Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
Katika hotuba yake Waziri Jafo amemtaka Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam Mhe. Omary Abdallah Matulanga kuongoza Jiji bila ya kujali kundi fulani la watu, "Jiji litakwenda vizuri au litakwenda vibaya ni la kwako, ila naamini litakwenda vizuri’’, Alisema Jafo.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.