Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa (Mb) amewaelekeza Maafisa kutoka Wizara hiyo kuhakikisha wanafanyia kazi suala la urasimishaji wa Ardhi Mkoa wa Dar es Salaam kwani migogoro ya ardhi imekua mjadala mkubwa katika Mkoa huo.
Mhe. Silaa ametoa maelekezo hayo leo tarehe 04 Oktoba, 2023 wakati wa kikao cha Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam kujadili changamoto za ardhi zinazokabili Halmashauri tano za Mkoa wa Dar es Salaam.
Akizungumza katika Kikao hicho Mhe. Silaa amesema “Kazi kubwa ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma Muhimu kwa ukaribu zaidi hivyo ili kutimiza maono ya Rais wetu ni wajibu kuhakikisha tunapanga, tunapima na tunarasimisha ardhi kwa Wananchi wetu kama Ilani ya Chama inavyoelekeza hivyo niwahakikishie kutokana na kikao hichi changamoto zote za migogoro ya Ardhi katika Mkoa wetu zinaenda kupatiwa ufumbuzi na natoa siku Saba kwa maafisa kutoka wizara ya Ardhi kuniletea taarifa za urasimishaji wa Ardhi katika Mkoa wa Dar es Salaam ambapo kutokana na taarifa hiyo utekelezaji wa kukabiliana na migogoro ya ardhi kwenye Halmashauri zetu utaanza kuchukuliwa hatua stahiki.”
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Segerea Mhe. Bonnah Kamoli ameishukuru Kamati ya Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Dar es Salaam kwa kuandaa kikao hichi chenye tija ya kutatua migogoro ya Ardhi kwa Wananchi huku akieleza kuwa suala la urasimishaji katika Jimbo la Segerea limekua changamoto hususani kata ya Kisukuru hivyo ameiomba Serikali kushirikiana na Wizara husika kutatua changamoto hiyo.
Naye Mwenyekiti wa Mipango Miji na Mazingira Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Mhe. Nyansika Getama ambaye ni Diwani wa Kata ya Kivule ameeleza kuwa maeneo mengi ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam hayajafanyiwa urasimishaji jambo ambalo limekua likileta migogoro ya mipaka ya ardhi kwa Wananchi wa Jiji la Dar es Salaam hivyo ameiomba Wizara ya Ardhi kushirikiana na wataalamu kutoka Halmashauri ili kuweza kurasimisha maeneo hayo.
Awali akifungua kikao hicho Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Dar es Salaam Ndg. Abasi Zuberi Mtemvu ameeleleza kuwa migogoro ya Ardhi katika Halmashauri za Mkoa wa Dar es Salaam imekua janga kubwa kwani maeneo mengi ya Mkoa wa Dar es Salaam hayajapimwa wala kurasimishwa.
“Tumefanya Kikao hichi kwa Mara ya Kwanza na Waziri wa Ardhi kwani ndiye mwenye dhamana ya suala hili na kwakua tumejionea migogoro ya ardhi ikikabili Halmashauri zetu hii Ndio sababu ya kumualika Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwenye kikao hichi ili kuweza kusikiliza changamoto zote za ardhi za Mkoa wetu na kutupatia ufumbuzi juu ya changamoto hii.” Ameeleza Ndg. Mtemvu
Aidha kikao hicho cha Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Dar es Salaam kiliweza kuhudhuriwa na Wakuu wa Wilaya zote za Mkoa wa DSM, Makatibu Tawala, Wakurugenzi, Maafisa Ardhi kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na Maafisa Ardhi kutoka Halmashauri zote za Mkoa wa Dar es Salaam.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.