Na : Doina Mwambagi
Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam leo Februari 18, 2025 imeingia makubaliano ya utiaji saini wa mikataba mitatu muhimu yenye lengo la kuboresha huduma za Jamii na usalama wa wakazi Jiji hili.
Mikataba hiyo ni umaliziaji wa Shule ya Sekondari ya Bonyokwa, ufungaji wa kamera za usalama (CCTV cameras) katika Soko la Kariakoo, pamoja na mkataba wa uzoaji wa taka katika masoko ya jiji la Dar es pamoja makabidhiano ya malori matano ya uzoaji taka.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, ndugu Elihuruma Mabelya amesema kuwa uongozi wa Halmashauri hautawavumilia wakandarasi wanaochelewesha Miradi hiyo.
"Hatutawafumbia macho wakandarasi watakaozembea au kuchelewesha miradi hii, tunataka kuona utekelezaji unafanyika kwa kasi na viwango vya juu ili wananchi wapate huduma bora," alisema Mabelya.
Aidha, Mkurugenzi Mabelya amesema kuwa ufungaji wa kamera za CCTV katika Soko la Kariakoo ni hatua muhimu katika kuimarisha usalama wa wafanyabiashara na wateja, ikizingatiwa kuwa soko hilo ni kitovu cha biashara Jijini na hatua hii inatarajiwa kusaidia kudhibiti matukio ya wizi, uhalifu, na kuimarisha usimamizi wa eneo hilo.
Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa halmashauri ya jiji la Dar es salaam, wadau wa maendeleo, na wawakilishi wa kampuni zinazohusika na miradi hiyo.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.