Taasisi za Umma nchini zimeagizwa kuzingatia viwango vyote vya usalama katika mifumo ya TEHAMA wakati wa kubuni, kusanifu, kujenga, kusimika na kuendesha mifumo hiyo, badala ya kujenga mfumo kwanza na unapokamilika ndipo masuala ya usalama wa kufikiriwa.
Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa kwenye ufunguzi wa Kikao Kazi cha Pili cha Serikali Mtandao kwa kundi la Makatibu Wakuu na Maofisa Masuuli wa Serikali Kuu na Mamlaka ya Serikali za Mitaa uliofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Sayansi ya Kompyuta, Habari na Mawasiliano "UDOM-CIVE" jijini Dodoma Februari 1, 2019.
Dkt. Mwanjelwa amesema, tatizo la usalama mitandaoni linazidi kukua kadri maendeleo ya Teknolojia yanavyozidi kukua na hivyo, bila kukabiliwa kikamilifu, litaathiri kwa kiasi kikubwa jitihada zilizokwishafanyika katika eneo la Serikali Mtandao.
“Njia mojawapo ya kujihakikishia usalama, ni kuhakikisha utengenezaji wa mifumo yetu unazingatia programu ambazo watalaam wetu wanaweza wakatambua kinachofanyika badala ya kuwa na mifumo ambayo hatujui kinachoendelea nyuma ya pazia”, amesisitiza Dkt. Mwanjelwa
Pia, amezihimiza Taasisi zote za Umma kuendelea kushirikiana na Wakala ya Serikali Mtandao “e-GA” kila zinapobuni na kutekeleza miradi ya TEHAMA ili kuondoa urudufu wa miradi na raslimali za TEHAMA miongoni mwa Taasisi za Serikali.
“Hatuwezi kuendelea kufanya kama tulivyofanya hapo awali kabla ya kuanzisha Wakala hii”. Ni ukweli usiopingika kwamba hakuna sekta yoyote iliyoendelea bila kuratibiwa, kwa hiyo ni vema tukazingatia miongozo mbalimbali inayotolewa katika kutekeleza Serikali Mtandao.
Aidha, Dkt. Mwanjelwa amesema kuwa, iwapo utekelezaji wa mifumo na miundombinu ya TEHAMA utawianishwa na kuwezesha ubadilishanaji wa taarifa ndani ya Taasisi za umma na baina ya Taasisi za umma, utoaji wa huduma kwa njia ya mtandao utakuwa ni kichocheo muhimu katika kufikia maendeleo ya viwanda.
Kikao cha Pili cha Serikali Mtandao kimefanyika kuanzia Januari 30 hadi Februari 2, 2019 na kuhusisha zaidi ya watumishi wa umma 700 kutoka Taasisi mbalimbali Serikalini.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.