Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za mikoa Serikali za Mitaa Mhe. Deogratius Ndejembi (Mb) amewaagiza Wakuu wa Mikoa, Wilaya pamoja na Wakurugenzi wote nchini kuhakikisha wanafanya tathmini za maeneo yao hususani maeneo ya Biashara ili kujiweka tayari kukabiliana na majanga ya moto huku akiwataka kushirikiana na Mamlaka ya Maji Safi na Mazingira namna gani hatua za dharura zinaweza kuchukuliwa endapo likitokea janga la moto ambapo kwa upande wa Dar es Salaam wanatakiwa kushirikiana na DAWASA wanapofanya tathmini za maeneo yao ya Kibiashara kuepukana na janga la moto.
Mhe. Ndejembi ameyaelekeza hayo leo Oktoba 3, 2023 kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa (Mb) wakati wa ziara yake ya kukagua eneo la Wafanyabiashara lililoungua na moto siku ya Jumapili Oktoba 1, 2023 maeneo ya Big Bon - Kariakoo Jijini Dar es Salaam.
Aidha Mhe. Ndejembi amewataka wafanyabiashara kuwa wavumilivu hadi Kamati ya uchunguzi iliyoundwa kutoa taarifa za moto kukamilisha uchunguzi juu ya chanzo cha moto huo.
“Niwaombe Wafanyabiashara mliopatwa na janga hili la moto kuwa wavumilivu hadi Kamati ya Siku Saba iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa kutoa taarifa juu ya moto huo kukamilika na pindi taarifa hiyo itakapotolewa hatua stahiki zitachukuliwa papo hapo kwani Serikali yetu inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni sikivu na inafanya utekelezaji maramoja hivyo tuwe wasikivu na wavumilivu hadi taarifa hiyo itakapotolewa kwani siku Saba sio nyingi na Mpaka kufikia leo zimebaki takribani siku nne taarifa hiyo ikamilike.”
Awali akizungumza katika eneo hilo Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo ametoa shukrani zake kwa Jeshi la Polisi pamoja na Jeshi la Zima Moto kwa juhudi walizozionesha Mpaka kuzima moto huo huku akiahidi kutekeleza yale yote aliyoagiza Mhe. Ndejembi.
“Napenda kulishukuru Jeshi la Polisi kwani pindi moto unawaka waliweza Kudhibiti Hali hiyo na watu waliokoa vitu vyao na maduka mengine hayakuweza kuibiwa, pia niwashukuru Jeshi la Zima Moto kwa uwepesi wao hadi kufanikiwa kuzima moto huo na kupunguza madhara hivyo tunasubiri taarifa ya Kamati iliyoundwa ili tuweze kujua Chanzo cha moto huo na hatua nyingine zitafuata.”
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.