Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo amewataka viongozi wa Kata na Mitaa kutenda haki katika utoaji wa mikopo ya asilimia 10 inayotarajiwa kutolewa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam hivi karibuni.
Wito huo umetolewa leo Desemba 10, 2024 Na Mkuu huyo wa Wilaya katika halfa ya Uapisho wa Uajibikaji na Uadilifu katika Utoaji na usimamiaji wa Mikopo ya asilimia 10 kwa wajumbe wa kamati za huduma ya mikopo ngazi ya Kata katika Halmshauri ya Jiji la Dar es Salaam .
Akiongea na wajumbe hao, Mhe. Mpogolo amesema lengo la Mikopo hiyo ni kuwawezesha makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ili waweze kujikwamua kiuchumi.
"Niwaombe wajumbe wa kamati ya mikopo ngazi ya Kata mkatende haki kwa kutoa Elimu na Mikopo kwa walengwa kwa kuzingatia vigezo na kanuni za mikopo na si vinginevyo”. Alisema Mhe. Mpogolo.
Aidha, Mhe. Mpogolo amekabidhi spika 36 kwa Watendaji wa Kata za Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam lengo likiwa ni kufikisha Elimu ya mikopo kwa Wananchi huku akiwataka kutumia vifaa hivyo kwa kazi husika na si kwa matumizi binafsi.
Naye Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam Mhe. Omary Kumbilamoto amewataka wajumbe wa kamati ya kusimamia na utoaji wa Mikopo ngazi ya kata kuhakikisha wanazingatia sheria, kanuni na taratibu na miongozo ya Utoaji wa mikopo hiyo.
Hatua hiyo ya uapisho ni muendelezo wa maandalizi ya utoaji wa mikopo hiyo ya asilimia 10 ambapo makundi mbalimbali yamekuwa yakipatiwa mafunzo sambamba na viapo ili kuweza kuwahudumia wananchi kwa haki na uwazi.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.