Mratibu wa Magonjwa yasiyoambukiza Jiji la DSM Dkt. Milka Mathania amewataka wakazi wa Jiji hilo kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza kwa kubadili mitindo na mienendo isiyofaa ya maisha, ili kuwa na Taifa lenye afya bora.
Dkt. Mathania ameyasema hayo leo Novemba 11, 2024 wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Magonjwa Yasiyoambukiza yenye kaulimbiu isemayo "Muda ni sasa, zuia magonjwa yasiyoambukiza, mahali pa kazi" yaliyofanyika kwenye Kituo cha Afya Kinyerezi na kuwasihi kuacha mienendo isiyofaa ikiwemo kutofanya mazoezi, ulaji usiofaa, ulevi na uvutaji sigara kwani vimekua ni sababu kuu za kuchangia kuenea kwa magonjwa yasiyoambukiza.
"Magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo shinikizo la damu, magonjwa ya moyo, saratani na kisukari yamekuwa chanzo cha vifo na usumbufu kwa wananchi wa maeneo ya mijini ikiwemo Mkoa wa Dar es Salaam na kwa kulitambua hilo, Serikali inaendelea kutoa elimu ya kutosha ya namna bora ya kukabiliana na magonjwa hayo na kuendelea kuboresha na kuongeza miundombinu mbalimbali ya afya.
Hivyo kupitia wiki hii ya maadhimisho, wananchi watapata fursa ya kupima magonjwa mbalimbali bure na kupatiwa ushauri wa kitaalamu." Ameongeza Dkt. Mathania.
Huduma zinazotelewa kwenye wiki ya magonjwa yasiyoambukiza ni pamoja na Uchunguzi wa Saratani ya shingo ya kizazi, huduma ya kinywa na meno, huduma ya upimaji wa macho, upimaji wa kisukari, upimaji wa shinikizo la damu pamoja na lishe, urefu na uzito na huduma zinatolewa kwenye Vituo vyote vya Afya bila malipo.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.