Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam leo tarehe 9 Novemba, 2023 wamefanya mkutano wa Robo ya Kwanza ya Mwaka wa Fedha 2023/2024 (Julai – Septemba 2023) katika ukumbi wa Arnatoglou na kupitisha taarifa ya utendaji kazi kwa robo hiyo.
Aidha, katika kikao hicho Wenyeviti wa Kamati za kudumu za Halmashauri wamewasilisha taarifa za kamati zao na wajumbe wa Baraza la Madiwani wamezipokea na kuzipitisha Ili zibaki kuwa kumbukumbu sahihi kwa Halmashauri
Katika kikao hicho, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imewasilisha taarifa ya uwekezaji wa shirika la DDC linaloingia ubia na Tosh Logistics Company kwa muda wa miaka 25 ambapo Wanatarajia kufanya ujenzi wa jengo la ghorofa 6 katika eneo la Kariakoo lenye thamani ya Shilingi Bilioni 37.3 ambalo litakua na jumla ya maduka 398, stoo 36, baa na kumbi 10 ambapo Mradi huu utakua ni wa Jenga, endesha, rejesha na baada ya miaka 25 unatarajiwa kuwa umeingiza mapato ya bilioni 121 ambapo Bilioni 84 ikiwa ni faida na Bilioni 37 ikiwa ni gharama za jengo.
Aidha, katika kikao hicho Kamishina Msaidizi wa Ardhi Ndg. Shukurani Kyando alipata wasaa wa kuwaelezea Madiwani urasimishaji wa Ardhi na Makazi kwa Jiji hilo ikiwa ni moja ya Agenda ya Kikao hicho na kusema “Kutokana na changamoto mbalimbali za urasimishaji wa Ardhi, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya Dunia imekuja na suluhisho kwa kuwasaidia wananchi kwa kuwasogezea huduma ya urasimishaji wa ardhi na makazi katika mitaa yao, ambapo watendaji wa Halmashauri na Kamishina wa Ardhi wataweka kambi ya siku 25 katika mitaa husika ambapo Wananchi watapata huduma ya kupanga, kupimiwa ardhi pamoja na kupewa hati za umiliki kwa muda wa siku moja.”
Sambamba na hilo, Mkurugenzi wa Halamashauri ya Jiji la Dar es salaam Ndg. Jomary Satura amewaahidi kufanya kazi kwa bidii kwa kufata maelekezo ya Meya na Baraza la Madiwani.
Akifunga kikao hicho Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam Mhe. Omary Kumbilamoto amewashukuru Waheshimiwa Madiwani na Watendaji wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa kushiriki katika ziara za kamati mbalimbali za robo ya kwanza 2023/2024. Kwani wamefanya kazi kwa kushirikiana kwa lengo la kuwaletea maendeleo wananchi.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.