Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam Mhe. Albert Chalamila amekabidhi msaada wa gari la kubebea wagonjwa (ambulance) na vifaa tiba wenye thamani ya takribani TZS. Mil 188 kwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Amana kutoka Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) wenye lengo la kusaidia kuboresha utoaji wa huduma za magonjwa ya dharura na ajali hospitalini hapo.
Akikabidhi msaada huo Mhe. Chalamila amesema Mkoa wa Dar Es Salaam ndio Mkoa ambao unaidadi kubwa ya watu kuliko mikoa mingine nchini na Hospitali ya Amana ipo katikati ya Jiji na imekuwa ikihudumia idadi kubwa ya wagonjwa wa dharura na ajali hivyo msaada huu utasaidia kuimarisha huduma za dharura hospitalini hapo.
“Nawapongeza wadau hawa kwa kuamua kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuboresha huduma za afya nchini, msaada huu utasaidia kuendelea kuboresha utoaji wa huduma za dharura kwa wakazi wa mkoa huu” amesema Mhe. Chalamila
Akipokea msaada huo Mganga Mfawidhi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Amana Dkt. Bryceson Kiwelu ameishukuru Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka kwa kuendelea kuunga mkono uboreshaji wa huduma za dharura hospitalini hapo kwa kutoa msaada ambao utasaidia kuokoa maisha ya wagonjwa.
“Idara ya Magonjwa ya Dharura Hospitali ya Amana imejitosheleza katika nyanja zote na inatoa huduma za dharura ndani na nje ya hospitali, tuna wataalam wabobezi wenye uzoefu wa kutoa huduma za dharura kuanzia eneo la tukio hadi hadi mgonjwa anapofikishwa hospitali hivyo tunawashukuru wadau hawa kwa kuendelea kutuongezea nguvu katika Idara hii” amsema Dkt. Kiwelu
Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka imekuwa ikishirikiana kwa ukaribu na Hospitali ya Amana ambapo hivi karibuni imewaleta baadhi ya wataalam wakiwemo Madaktari Bingwa wa Magonjwa ya Dharura, Wauguzi na Madereva ambao watasaidia kuongeza nguvu kazi ya utoaji wa huduma pamoja kuendesha mafunzo kwa watumishi juu ya namna ya kujiandaa na kukabiliana na magonjwa ya dharura na mlipuko punde yanapotokea.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.