Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo asisitiza upatikanaji wa haki za wazee katika kupata huduma za afya hayo ameyasema leo Oktoba 13, 2023 wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani yaliyofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja yaliombatana na kauli mbiu isemayo ‘Uthabiti wa Wazee kwenye Dunia yenye Mabadiliko’.
Akiongea wakati wa hafla hiyo Mhe. Mpogolo ameeleza kuwa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya kwa kushirikiana na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam watazingatia haki za wazee na wananchi wote wanaowahudumia.
“Sisi kama sehemu ya huduma kwa Watanzania tutahakikisha tunazingatia haki kwa wazee na watu wote tunaowahudumia kama Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anavyotaka na tutahakikisha tunaboresha huduma za afya kwa wazee wetu kwa kuwapatia kadi za matibabu pamoja na upatikanaji wa dawa hivyo nitoe wito kwa Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kuhakikisha dawa muhimu za magonjwa yanayowasumbua wazee zipo katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya ili wapate matibabu ya uhakika katika vituo hivyo kwani Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amewekeza zaidi ya Shilingi Bilioni 20 kaajili ya uboreshaji wa huduma za afya na miundombinu hivyo tuhakikishe tunaunga mkono juhudi zake."
Sambamba na hilo Mhe. Mpogolo alikabidhi vitambulisho 360 vya bima ya ICHF kwa waze huku akiwaahidi wazee kuwa wavumilivu kwani Halmashauri itaendelea kutoa vitambulisho vya matibabu kwa ajili yao sambamba na kumuagiza Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kuona namna gani wazee watashirikishwa kuhudhuria vikao vya baraza.
Awali akitoa taarifa ya usimamizi na uratibu wa shughuli za dawati la wazee kwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Mratibu wa dawati la Wazee Bi. Millen Makundi ameeleza kuwa dawati la wazee limekua likitekeleza majukumu yote kwa mujibu wa Sera ya Taifa ya Mwaka 2003 yenye mpangomkakati wa kuzuia na kupambana na mauaji ya wazee Tanzania pamoja na kutekeleza sera ya misamaha ya matibabu kwa wazee wenye umri wa miaka 60.
Aidha Bi. Makundi ameeleza kuwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ina jumla ya wazee 21,175 kati yao wanaume 10,058 na wanawake 11,117 ambapo wazee 18,613 wamepewa vitambulisho huku wazee 2345 wakiweza kupatiwa bima za afya za ICHF.
Akitoa shukrani zake kwa Mkuu wa Wilaya ya Ilala pamoja na viongozi wote wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Baraza la wazee Wilaya ya Ilala Bw. Salim Matimbwa ameshukuru uboreshwaji wa huduma za matibabu kwa wazee huku akiomba ofisi ya Mkurugenzi kushirikishwa kwenye baraza la madiwani pamoja na vikao vingine vinavyohitaji ushiriki wa wazee.
Maadhimisho haya Kitaifa yamefanyika tarehe 06 Oktoba 2023 Mkoani Geita huku kwa upande wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam yakifanyika Leo Oktoba 13 yakiwa yameambatana na Siku ya Macho Duniani yenye kauli mbiu isemayo ‘Penda Macho yako mahali pa kazi’ sambamba na siku ya watu wenye ugonjwa wa akili na kauli mbiu isemayo ‘Afya ya Akili ni haki kwa binadamu wote’
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.