Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mheshimiwa Ngw'ilabuzu Ludigija leo tarehe 21Julai, 2022 amefanya kikao kazi na watendaji wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam lengo likiwa ni kuwakumbusha watendaji hao wanahakikisha wanasimamia majukumu yao kwa kuhakikisha wanadhibiti zoezi la biashara holela, wanasimamia usafi pamoja na kuhakikisha maegesho ya bajaji, bodaboda na guta zinazoingia katikati ya Mji wanaegesha vyombo hivyo katika vituo maalumu walivyopangiwa.
Kikao kazi hicho kilichofanyika katika ukumbi wa Arnatoglou uliopo Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam kilihudhuriwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama, Wakuu wa Idara na Vitengo wa Halmashauri ya Jiji la DSM watendaji wa Mitaa, Wenyeviti wa Mitaa, Wenyeviti wa Wamachinga, bodaboda, bajaji pamoja na wadau mbalimbali.
Aidha katika kikao kazi hicho Mheshimiwa Ludigija ametoa maelekezo kwa watendaji wote wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kuhakikisha wanasimamia vyema zoezi la ufanyaji biashara kwani wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama machinga wameanza kurudi kufanya biashara katika maeneo yasiyo rasmi ambapo wanasababisha uchafu wa mazingira.
"Tumefanya kazi kubwa kuwapeleka wafanya biashara kwenye maeneo rasmi ambapo nia ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ni kuwawezesha wafanyabiashara wakiwa katika maeneo rasmi hivyo nielekeze wafanyabiashara wote ambao wamerudi kufanya biashara holela warudi kwenye maeneo yao rasmi tuliyowapanga Hivyo Wenyeviti wa Serikali za mitaa tuhakikishe mnatekeleza hili ili tuweze kuendana na kauli mbiu ya 'Safisha, pendezesha, Dar es Salaam ili tuwe na sura nzuri ya Jiji la Dar es Salaam."
Sambamba na hilo Mheshimiwa Ludigija ameendelea kusema "Haiwezekani Mkuu wa Wilaya nifanye majukumu yangu na pia nifanye majukumu yako Mtendaji wa Kata hivyo naomba mhakikishe mnasimamia na kutekeleza vyema majukumu yenu ya kazi."
Aidha Mheshimiwa Ludigija amewataka watu wa maegesho kuhakikisha wanakusanya ushuru wa maegesho katika maeneo husika kwani ushuru wa maegesho umekua ni kero kwa Wananchi hivyo amewataka wakusanya ushuru wa maegesho wakusanye ushuru maeneo yao husika pia amewataka bodaboda wote, bajaji pamoja na watu wa maguta kupaki katika vituo tisa walivyopangiwa na sio kupaki holelaholea.
Akihitimisha kikao hicho Mheahimiwa Ludigija amesema "Niwaombe mfanye yote niliyowaelekeza na wenyeviti wa Mtaa tusaidiane kutekeleza kauli mbiu ya mkuu wa mkoa ya SAFISHA, PENDEZESHA DAR ES SALAAM hivyo niwakumbushe kuwa usafi wa mwisho wa mwezi huu utakaofanyika tarehe 30 utafanyika katika maeneo ya ‘Smart Area’ hivyo tujiandae kufanya usafi kwa kuliweka Jiji letu safi.”
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.