Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo ameipongeza Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa kuendelea kuimarisha huduma za afya ikiwemo njia za upatikanaji wa dawa, vifaa tiba pamoja magari ya kubeba wagonjwa ili kuhakikisha huduma bora kwa wananchi zinatolewa kwenye vituo vya afya.
Hayo ameyasema leo Novemba 7, 2023 Katika viwanja vya ukumbi wa Arnatouglou Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam wakati akikabidhi Magari saba ya kubebea wagonjwa (Ambulance) kwa Mganga Mkuu wa Jiji ambayo yamekarabatiwa kwa kutumia fedha za mapato ya ndani ya Idara ya Afya shilingi milioni 24 baada ya kukaa muda mrefu bila matengenezo.
“Magari haya ambayo yatakua msaada mkubwa wa kuimarisha huduma za afya yanatakiwa yatunzwe kwani Mheshimiwa Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anataka tusimamie miradi vizuri na kwa kuacha alama kwa wananchi hivyo niwapongeze kwa kutumia vyema fedha za mapato ya ndani kwa kukarabati magari ya kubebea wagonjwa na kuhakikisha huduma za afya zinaboreshwa katika Halmashauri yetu. Hii ni alama kubwa sana aliyoionesha Mkurugenzi wa Jiji kwa kushirikiana na wataalamu wake kuhakikisha huduma za afya zinaboreshwa na wananchi wanapata huduma bora kwa wakati." Ameeleza DC Mpogolo.
Awali Akizungumza katika hafla hiyo Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam Ndg. Jomaary Satura ameeleza kuwa ataendelea kusimamia vizuri mapato ya Halmashauri ili kupitia mapato hayo miradi mbalimbali iweze kuboreshwa huku akimpongeza Mganga Mkuu wa Jiji kwa kazi nzuri anayoifanya ya kuhakikisha sekta ya afya katika Jiji la Dar es Salaam inaimarika zaidi.
Akipokea magari hayo Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Dkt. Zaituni Hamza ameeleza kuwa “Katika kuelekea 2024 sisi kama Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam tutahakikisha tunaendelea kuboresha huduma za afya kwa wananchi ambapo tumeweza kutenga shilingi milioni 100 kwenye Makusanyo ya shilingi milioni 500 ya Idara ili kukarabati magari ya wagonjwa yaliyokuwa hayafanyi kazi kwa kipindi kirefu ambapo takribani magari 7 ya kubebea wagonjwa tunayokabithiwa leo yamekarabatiwa kwa shilingi milioni 24 fedha kutoka mapato ya ndani ya Idara ya Afya hivyo niwahakikishieni kwa kushirikiana na wataalamu wenzangu tutaendelea kuboresha huduma za afya katika Jiji letu hata hivyo tumejipanga kujenga chuo kuku cha Kati katika Halmashauri yetu lengo ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora kwa wakati”.
Sambamba na hilo Dkt. Zaituni amehakikisha kusimamia magari hayo ili yaweze kudumu kwa muda mrefu huku akieleza kuwa kutokana na mapato ya ndani ya Halmashauri, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imeanza utekelezaji wa jengo la upasuaji pamoja na wodi za Wanaume na Wanawake katika Hospitali ya Mnazi Mmoja hii ikiwa ni kuendelea kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa Jiji la Dar es Salaam.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.