Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo leo Oktoba 18, 2023 amefanya ziara ya kusikiliza na kutatua kero za Wananchi wa Kata ya Vingunguti pamoja naKata ya Mnyamani ikiwa ni utaratibu wake wa kuwafikia wananchi kusikiliza na kutatua kero zao.
Akiwa katika kusikiliza kero za wananchi wa Kata ya Vingunguti eneo la Mabuchani Mhe. Mpogolo amesema amebaini kero kubwa kutoka kwa wananchi wa Kata ya Vingunguti ni kukosekana kwa wataalamu wa ngozi hivyo kufanya watu wa mabucha kutupa ngozi hizo, ukosefu wa Dawa katika kituo cha Afya Buguruni, pamoja na ubovu wa huduma za kampuni za uzoaji taka.
Hata hivyo Mhe. Mpogolo amewataka Viongozi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam hususani Mkuu wa Divisheni ya Mifugo na Uvuvi kuhakikisha anatafuta wataalamu wa ngozi ili kuona namna gani ya kuboresha huduma ya ngozi pia amemtaka ahakikishe eneo la nje la machinjio linaboreshwa kuelekea katika msimu wa mvua.
“Niwaombe Viongozi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kuandaa kikao na wataalamu wa ngozi ili tuweze kuboresha huduma za ngozi kwani ngozi ina thamani kubwa na itatuingizia mapato hivyo na mimi nitashirikiana na Mstahiki Meya kutafuta wataalamu hao tuone namna gani watatuelekeza kuhusu uboreshaji wa ngozi hizo za wanyama pia tuhakikishe tunaboresha zaidi huduma katika machinjio yetu lengo likiwa ni kuzuia upotevu wa mapato yetu kwani Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ametenga fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya Elimu, Afya na Barabara hivyo mapato hayo yatasaidia katika utekelezaji wa miradi hiyo ya Maendeleo.” Amesema Mhe. Mpogolo
Kwa upande Mwingine Mhe. Mpogolo ameweza kusikiliza kero za Wananchi wa Mnyamani na kumuelekeza Mganga Mkuu wa Jiji la Dar es Salaam kuhakikisha huduma za afya katika kituo cha afya Buguruni zinaboreshwa hususani eneo la huduma kwa wateja kwani inaonekana wahudumu wa kituo hicho hawana huduma nzuri kwa wagonjwa wao.
Sambamba na hilo, Mhe. Mpogolo amewataka Wananchi wa Kata ya Mnyamani pamoja na vingunguti kutoa ada za taka na pia kuwa wavumilivu kwani suala la mkandarasi anaezoa taka maeneo hayo litafanyiwa kazi huku akiwataka Wananchi hao kufika ofisini kwake pindi wanapokua na malalamiko.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam aliweza kumuhakikishia Mkuu wa Wilaya kutekeleza yote aliyowaagiza ili kuboresha huduma na kuzuia upotevu wa mapato ya Halmashauri.
Mwisho wananchi na viongozi wa Kata za Mnyamani na Vingunguti wamepongeza ziara ya Mkuu wa Wilaya kwa kuwakumbuka katika kusikiliza kero zao na kumuhakikishia kutekeleza yote aliyoyaagiza. Ziara hii ni endelevu kwa kata zote 36 za Ilala.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.