Na: Shalua Mpanda
Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mheshimiwa Edward Mpogolo amefanya ziara ya kukagua maeneo mbalimbali yaliyoathiriwa na mvua zinazoendelea kunyeesha huku akitoa onyo kwa wale waliojenga na kufanya shughuli za kilimo pembezoni mwa mito.
Akiwa ameambatana na Mkurugenzi wa Jiji la Dar es salaam ndugu Elihuruma Mabelya, Mkuu huyo wa Wilaya ametembelea katika eneo la daraja Mzinga ambalo sehemu ya daraja hilo lilikatika na kusababisha kukatika kwa mawasiliano kati ya Kata za Mzinga na Kivule.
Mhe. Mpogolo amekemea baadhi ya wananchi ambao wameamua kujimilikisha maeneo ya pembezoni mwa vyanzo vya maji huku akisisitiza wafuate Sheria ambayo inawataka kufanya shughuli hizo mita 60 kutoka kwenye vyanzo hivyo.
"Niwatake wenyeviti wangu wa Mitaa na Watendaji wahakikishe wanasimamia suala hili kwa kuwa hata haya mafuriko tunayoyaona mengi yamesababishwa na watu kuzuia njia za maji hivyo maji kutafuta njia nyingine ya kupita". Alisema.
Mbali na daraja hilo, Mkuu huyo wa Wilaya alitembelea eneo la kata ya Majohe mtaa wa Maguruwe ambapo pia alijionea jinsi mvua hizo zilivyoharibu miundombinu ya barabara hiyo na kusababisha adha kwa watumiaji wa barabara hiyo.
Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) imetoa tahadhari kuhusu uwepo wa mvua kubwa katika maeneo mengi nchini hivyo wananchi hawana budi kuchukua hatua stahiki zikiwemo kuhama katika maeneo ya mabonde ili kuepusha maafa yanayoweza kutokea endapo yakitokea mafuriko katika maeneo hayo.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.