Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo amewataka Wafanyabiashara wa Kariakoo kuwa wazalendo kwa kuhakikisha wanashirikiana na Serikali kuwapanga wafanyabiashara ndogondogo (machinga) katika maeneo sahihi bila kuzuia biashara nyingine na njia za watembea kwa mguu pamoja na kuwatambua wafanyabiashara wote ambao sio machinga ila wameweka meza kama machinga kwa lengo la kukwepa kodi.
Mhe. Mpogolo ametoa maagizo hayo leo Juni 13, 2024 wakati wa kikao kazi na Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo kilichofanyika a katika ukumbi wa Arnatouglou Jijini Dar es Salaam kilicholenga kuwasilisha kero za wafanyabiashara hao.
Akiongea na Wafanyabiashara hao Mhe Mpogolo amesema “Kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam nina wajibu wa kusimamia na kushiriki katika kutatua changamoto zenu zinazowakabili kwani changamoto zote nimezichukua na nitakwenda kuzisimamia ziweze kutekelezwa kwa wakati zaidi hivyo niwaombe muwe watulivu kwani Serikali yetu iliyoko Chini ya Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ni sikivu na inawajali wafanyabiashara itahakikisha changamoto hizi zinatatuliwa kwani tumeanza kuweka taa baadhi ya maeneo ili kuhakikisha biashara zinafanyika masaa 24. Pia, niwaombe Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuendelea kutoa elimu ya kodi kwa wafanyabiashara ili kutengeneza ufahamu kwa wafanyabiashara lakini pia niwatake Jeshi la Polisi wafuate maelekezo ya Waziri Mkuu ambayo aliyatoa juu ya kamatakamata”.
Sambamba na hilo, Mhe. Mpogolo amewapongeza Wafanyabiashara kwa kuwa walipa kodi wazuri kwa Serikali huku akiwataka kuendelea na vikao vya mara kwa mara ambavyo vitakua na matokeo chanya ya kujenga pamoja na kukumbushana yote yanayosahaulika bila kusahau kukumbushana kujisajili.
Awali wakiwasilisha kero kwa Mhe. Mpogolo, wafanyabiashara wa Kariakoo wameeleza kuwa wafanyabiashara ndogondogo (wamachinga) ni lango la kutorosha mapato ya serikali, kwa kuwa kuna wafanyabiashara wakubwa Karikaoo ambao wamekuwa wakifunga maduka na kusambaza mizigo yao kupitia wamachinga huku wakionyesha kutoridhishwa na namna Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inavyowatendea hasa kwenye ushuru.
Akitoa Shukrani zake kwa Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo Ndg. Martin Mbwana amesema “Nipende Kukushukuru Mkuu wa Wilaya kwa kuitikia wito wetu na kuja kuongea na sisi ila ningeshauri kwamba hatua madhubuti zinapaswa kuchukuliwa ili kukabiliana na hali ya wamachinga ambao wamekua wakikwepa kodi."
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.