Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo, amefanya uzinduzi wa Wiki ya Chanjo mapema leo katika Kituo cha Afya Kitunda kilichopo Kata ya Kitunda.
Uzinduzi huo uliofanyika leo ni wa chanjo ya polio kwa watoto, zoezi lililosimamiwa na Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, wataalam wa Afya ya Mama na Mtoto kutoka Kituo cha Afya Kitunda pamoja na Wadau kutoka Shirika la Usimamizi na Uboreshaji wa Huduma za Afya (MDH)
Akizungumza na Wazazi waliohudhuria zoezi hilo litakalodumu kwa muda Wiki moja (24 Aprili, 2023 mpaka 30 Aprili, 2023) Mhe. Mpogolo amesema chanjo huokoa maisha ya mama na mtoto kwa kumkinga dhidi ya maradhi ambayo yanazuilika, na kuongeza kuwa kupata chanjo ni jambo la lazima kwavile inalinda pia kizazi kijacho dhidi ya magonjwa mbalimbali kama Surua na Polio.
“Ni wajibu na jukumu la kila Mzazi kuhakikisha mtoto wake anapata chanjo kwani ni muhimu kwa afya na inazuia watoto kupata ugonjwa wa kupooza. Pia Wakina Baba muwasindikize kliniki wake zenu na wasisitizeni wakina mama kuhakikisha wanapata chanjo zote kipindi cha ujauzito na wanapojifungua hakikisheni mtoto aliyezaliwa anapatiwa chanjo zote za utotoni ili kumlinda na maradhi kwani chanjo hizi ni salama na hazina madhara yoyote Kiafya”. Amesema Mhe. Mpogolo.
Chanjo dhidi ya ugonjwa wa Polio hutolewa mara nne yaani mara tu mtoto anapozaliwa, afikishapo wiki sita, wiki kumi na wiki 14 na wakati wa kampeni maalum zitakapohitajika.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.