Katika kutekeleza agizo la Serikali la kufanya usafi kila mwisho wa mwezi pamoja na kuendeleza na kutekeleza Kampeni ya Safisha, Pendezesha Dar es Salaam, leo Agosti 31, 2024 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imefanya zoezi la usafi katika Kanda namba 1, usafi uliofanyika kwenye fukwe za Dengu kuelekea daraja la Tanzanite .
Akiongea wakati wa zoezi hilo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Afisa Tarafa ya Kariakoo Bw. Adrian Kishe amewashukuru viongozi na wadau wote walioshiriki zoezi la usafi huku akitoa wito kwa wananchi kufanya usafi kama sehemu ya maisha yao ya kila siku .
“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amekua mstari wa mbele kuhakikisha mazingira yanatunzwa na kuwa safi ili kuepukana magonjwa ya mlipuko. Hivyo na sisi tuhakikishe tunafanya usafi wa mazingira kila siku katika nyumba zetu na mitaa tunayoishi hivyo tusisubirie jumamosi ya mwisho wa mwezi tu”
Awali akimkaribisha Mgeni Rasmi , Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam Tabu Shaibu ameeleza kuwa “Halmashauri yetu imeazimia kuhakikisha wananchi wanaishi katika mazingira bora na salama, Kama tunavyofahamu kuwa kiini cha magonjwa ya milipuko chanzo ni uchafu wa mazingira yanayomzunguka. Endapo Mazingira Yatakua machafu , binadamu na viumbe hai vitaathirika, Kama ilivyo ada kila mwisho wa mwezi lazima tufanye usafi katika mazingira yetu hivyo sisi Halmashari tumefanya usafi hapa Dengu Beach ili kulinda afya za wananchi wetu na pia viumbe hai wanaishi baharini.”
Sambamba na hilo, ameeleza kuwa jukumu la kutunza mazingira ni la wananchi wote hivyo tuachane tabia ya kutupa taka hivyo katika mazingira kwa ajili ya Afya zetu wenyewe na viumbe vinavyotuzunguka.
Aidha, Diwani wa Kata ya Kivukoni Mhe. Sharik Choughule amewapongeza na kuwashukuru viongozi, wadau, wananchi na taasisi mbalimbali waliojitokeza kufanya usafi katika beach hiyo.
“Mahali hapa ni sehemu mojawapo ambayo inatumiwa na wananchi kutoka sehemu mbalimbali kwa ajili ya mapumziko na mazoezi hivyo kwa kitendo hiki cha kusafisha mazingira haya ni kitendo cha uungwana na cha kuigwa, hivyo nitoe Shukrani zangu za dhati kabisa kwenu viongozi , wananchi na wadau wote kwa usafi mlioufanya." Amesema Mhe. Choughule.
Kwa upande wake Mkuu wa kanda namba moja Athumani Mtauka amesema kuwa jambo la usafi ni jambo la muhimu katika mazingira yetu na Afya zetu na kuahidi kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha mazingira yanakua safi na salama.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.