Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imetoa mafunzo ya siku mbili kwa vikundi 117 vya wajasiriamali wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 21-22 Novemba, 2019 kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kutumia vema na kurejesha mikopo ambayo Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kila mwaka huitoa kwa vikundi vya aina hiyo.
Mikopo hiyo inatokana na asilimia 10 ya Mapato ya Ndani yanayokusanywa na Halmashauri ya Jiji Dar es Salaam hutolewa kila mwaka kwa vikundi hivyo ili kuviwezesha kujikwamua kiuchumi, kujiongeza kipato na kupunguza tatizo la ajira kwa kujihusisha na shughuli mbalimbali za kiuchumi kwa ajili ya maendeleo ya Jiji la Dar es Salaam.
Akitoa mafunzo hayo, Afisa Maendeleo ya Jamii Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Bi. Margareth Mazwile amesema kuwa mikopo inayotolewa ina lengo la kuhakikisha wananchi wanajikwamua kiuchumi hivyo ni vyema wakatumia fursa ya kuchukua mikopo na kuitumia kikamilifu ili waweze kurejesha marejesho kwa wakati.
Katika mafunzo hayo Margareth Mazwile amewafundisha na kuwaelekeza jinsi ya kutumia mikopo hiyo kama ilivyokusudiwa na kujua namna ya kutafuta masoko katika biashara zao, uandaaji wa mipango ya biashara, uwekaji wa kumbukumbu pamoja na kufahamu namna ya uwekaji wa akiba.
Aidha, amevitaka vikundi vyote kuwa mabalozi wazuri kwa wananchi wengine ambao bado hawana muamko wa mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ambayo haina riba na kuendelea kuwasisitiza wanavikundi wote waliohudhuria mafunzo hayo kuhakikisha wanarejesha mikopo hiyo kwa wakati ili kupata nafasi ya kukopesheka zaidi na kutoa fursa kwa vikundi vingine kuweza kupata mikopo.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.