Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Suleimani Jaffo (Mb), leo tarehe 17 Machi, 2018 amekua mgeni rasmi katika uzinduzi wa shughuli za kukuza na kuutangaza utalii katika Jiji la Dar es Salaam.
Akizingumza katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na viongozi wa Serikali katika ngazi ya Mkoa, Waheshimiwa Madiwani, wadau mbalimbali katika sekta ya utalii na vikundi vya wajasiriamali vinavyoshughulika katika biashara ya utalii katika Jiji la Dar es Salaam, Waziri Jaffo ametoa pongezi kwa Halmashauri ya Jiji Dar es Salaam kwa jitihada inazozifanya za kukuza na kutangaza utalii nchini.
Aidha, ameziasa Mamlaka za Serikali za Mitaa kote nchini kuiga jitihada zinazofanywa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam katika kukuza na kuendeleza utalii nchini.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Paul C. Makonda amepongeza jitihada zinazofanywa na Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Jiji linaloongozwa na Mstahiki Meya wa Jiji pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji Dar es Salaam katika kukuza na kuendeleza utalii jijini pamoja na kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano katika kuwaletea Watanzania maendeleo.
Mhe. Paul Makonda amepiga marufuku baadhi ya watendaji Serikalini wanaozuia wasanii kurekodi video za nyimbo na sinema zao kwenye mandhari (location) mbalimbali za Jiji la Dar es Salaam kwani kwa kufanya hivyo inarudisha nyuma fursa za kutangaza na kukuza utalii wa Jiji la Dar es Salaam kupitia kazi za sanaa za wasanii hao.
Nae, Mstahiki Meya wa Jiji, Mhe. isaya Mwita Charles amesema Jiji la Dar es Salaam litashirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii, Chuo cha Taifa cha Utalii na wadau mbalimbali wa utalii ili kuhakikisha vivutio vingi vya utalii vinavyohusu historia ya nchi hii, mila, desturi na utamaduni, majengo ya kihistoria, siasa, uchumi na mambo ya jamii vinatangazwa ili kukuza utalii katika Jiji la Dar es Salaam na kuweza kutunza mazingira, kutoa ajira kwa wananchi wetu na pia kuchangia pato la Taifa.
Awali akiwasilisha taarifa ya mpango wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam katika kuendeleza utalii jijini Dar es Salaam kwa Waziri Jaffo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Bi. Sipora Liana ameeleza jitihada mbalimbali zilizofanywa na Halmashauri ikiwa ni pamoja na ununuzi wa mabasi ya kubeba watalii, uwekaji wa nembo malum katika majengo ya kihistoria, kuanzisha Kitabu cha Utalii kinachotoa taarifa mbalimbali ya vivutio, mahali pa kwenda, vitu muhimu vya kuangalia na taarifa za kiusalama ili kumrahisishia mgeni anapotembelea sehemu mbalimbali jijini pamoja na kutoa mafunzo kwa waongoza utalii (Tour Guides) watakaotumika kuongoza wageni na watalii watakaotoa taarifa sahihi za vivutio, historia ya Mji wakati wa kuwatembeza watalii kwenye vivutio mbalimbali.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.