Chanjo ya polio ni chanjo ambayo inatolewa kwa ajili ya kujikinga na virusi vya polio. Virusi hivi ni kati ya virusi ambavyo vinaleta ugonjwa wa kupooza, hivyo kusababisha mtu kushindwa kutembea, kuendelea na shughuli zake za kila siku na huathiri zaidi watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano.
Nchini Tanzania Serikali kupitia Wizara ya Afya iliendesha kampeni ya chanjo ya polio kwa watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano. Kampeni hiyo ilianza tarehe 18 Mei hadi 21 Mei, 2022.
Kampeni hii ilifanyika hapa nchini kutokana na maelekezo ya Shirika la Afya Duniani baada ya kubainika kuwepo kwa virusi vya polio nchini Malawi na kufanya mataifa ya jirani na nchi hiyo ikiwemo Tanzania kupata chanjo ya kujikinga dhidi ya ugonjwa huo.
Katika Jiji la Dar es Salaam, Mganga Mkuu wa Jiji la Dar es Salaam, Dr. Elizabeth Nyema, ametoa tathimini ya zoezi zima la utoaji wa chanjo na kusema kuwa katika kipindi cha siku nne za kampeni ya utoaji wa chanjo hiyo walitarajia kutoa chanjo kwa jumla ya watoto 221,201.
Alisema kuwa hadi kampeni hiyo ilipomalizika walifanikiwa kutoa chanjo kwa jumla ya watoto 266,908 ambayo ni sawa na asilimia 121. Hivyo kwa upande wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika zoezi hilo kwani muitikio wa wananchi ulikuwa ni mkubwa.
Dr. Nyema alisema kuwa hata baada ya kumalizika kwa siku nne za kampeni hiyo bado kuna baadhi ya wananchi waliojitokeza kuomba wapate chanjo hiyo kwa kuwa hawakufanikiwa kufikiwa na watoa huduma katika siku zile nne za kampeni. Kutokana na sababu hii Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam iliendelea kutoa chanjo hiyo kupitia vituo vyake vyote vya afya.
Dr. Nyema alisema kuwa wanawakinga watoto walio na umri wa chini ya miaka mitano kwa sababu katika umri huo huwa hawana kinga za kutosha ukilinganisha na wale wenye umri zaidi ya huo. Chanjo hiyo husaidia kuwakinga watoto wa rika hiyo ili wasipate maambukizi ya magonjwa mbalimbali ikiwemo ugonjwa wa polio.
Aidha, amewahakikishia wananchi wa Jji la Dar es Salaam kuwa chanjo zote zinazotangazwa na kutolewa na Serikali zimefanyiwa utafiti wa kina na ziko salama. Amewataka wananchi kujitokeza kupata chanjo hizo kwa wakati kwa ajili ya kujikinga na magonjwa mbalimbali hasa magonjwa ya mlipuko.
Dr. Nyema amewapongeza wananchi wote wa Dar es Salaam kwa kuendelea kufuata taratibu za afya na kutoa wito kuwa wahakikishe pale ambapo Serikali inatangaza kampeni mbalimbali waweze kuwa na mwitikio chanya na kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kupata chanjo hizo.
Amesema, “Tumetoka kwenye chanjo ya polio, tunaendelea na chanjo ya UVIKO 19 lakini pia kuna chanjo zile za watoto chini ya miaka mitano zinazoendelea vituoni, wananchi wahakikishe wanawafikisha watoto kupata chanjo hizo ili kuwakinga na magonjwa mbalimbali.”
Kampeni ya utoaji wa chanjo ya polio katika Jiji la Dar es Salaam ilitekelezwa kwa wataalamu wa afya kupita nyumba kwa nyumba, kwenye maeneo ya shule za watoto, masoko, maeneo ya mikusanyiko mikubwa ya watu na kwenye vituo vya kutolea huduma za afya. Hivyo, zoezi la utoaji wa chanjo hii lilifanikiwa kwa kiwango kikubwa kutokana na mwitikio mkubwa wa wananchi.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.