Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam leo Tarehe 19 Julai, 2023 imetoa taarifa kwa Umma na wadau kwa ujumla kupitia vyombo vya habari kuwa,imegawanya eneo la Jiji katika kanda za kiutawala ili kurahisisha utoaji wa huduma unaolenga kutoa huduma zenye ubora na usawa kwa jamii kwa kuzingatia utawala bora na kutumia kikamilifu rasilimali zilizopo.
Akitoa taarifa hiyo katika ukumbi wa mikutano wa Arnatoglou uliopo Mnazi Mmoja Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Bi.Tabu Shaibu amesema kuwa kuanzishwa kwa huduma za Kanda kutaongeza wigo wa ukusanyaji wa Mapato kwa kuwa ufuatiliaji wa walipa kodi utafanyika kwa ukaribu na ufanisi na kuiwezesha Halmashauri kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
Vilevile amesema kuwa kutasaidia kuweka mipango itakayozingatia mahitaji maalum ya maeneo tofauti kwa kuwa kila eneo linaweza kuwa na changamoto na mahitaji yake ya kipekee ,kugawa maeneo kutawezesha kubuni na kutekeleza programu zitakazozingatia mahitaji ya kila eneo.
Aidha ameongeza kuwa mpango huu utarahisisha ufanisi na usimamizi wa utoaji huduma kwa kuwa na eneo dogo ambapo kutasaidia kuimarisha usimamizi wa huduma za Umma na kusababisha utendaji kazi ulio bora na uwezo wa kurekebisha kwa haraka changamoto zinazojitokeza hivyo kuimarisha utekelezaji mzuri wa bajeti na mipango ya maendeleo.
Amesema, “Kuwepo kwa kanda kutasaidia kusikiliza na kutatua changamoto mbalimbali za wananchi kwa wakati kwa kuwa wakati mwingine matatizo ya wananchi yanashindwa kutatuliwa kwa wakati kwa sababu ya umbali wa kuzifikia huduma wanazozihitaji”
Bi. Tabu amesema kuwa kutakuwa na jumla ya Kanda 7 za kutolea huduma ambapo Kanda namba 1 ina Kata za Kivukoni, Kisutu, Upanga Mashariki na Upanga Magharibi na Ofisi ya Kanda itakuwa katika ofisi ya Kata Upanga Mashariki.
Kanda namba 2 ina Kata za Ilala, Mchikichini, Jangwani, Kariakoo, Gerezani na Mchafukoge, Ofisi ya Kanda itakuwa katika ofisi ya Kata Gerezani.
Kanda namba 3 inahusisha Kata za Buguruni, Mnyamani, Vingunguti, Kipawa, Minazi Mirefu na Kiwalani. Ofisi ya Kanda itakuwa katika Ofisi ya Kata ya Mnyamani .
Kanda namba 4 itajumuisha Kata za Tabata, Liwiti, Kimanga, Kisukulu, Segerea, Bonyokwa na Kinyerezi. Ofisi ya Kanda itakua katika Ofisi ya Kata ya Kinyerezi.
Kanda namba 5 itakuwa na Kata za Ukonga, Gongo la Mboto, Pugu Stesheni na Pugu na Ofisi ya Kanda hii itakuwa katika Ofisi ya Kata ya Gongo la Mboto.
Kanda namba 6 ina Kata za Kitunda, Mzinga, Kivule, Kipunguni na Majohe ambapo wananchi wa Kata hizi watahudumiwa katika Ofisi ya Kata ya Kipunguni.
Kanda namba 7 inahusisha kata za Buyuni, Chanika, Zingiziwa na Msongola ambapo Ofisi ya Kata ya Chanika itatumika kama Ofisi ya Kanda hii.
Vituo hivi vya kanda tayari vimekwishaanza kutoa huduma chini ya Uongozi wa Mameneja wa Kanda.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.