Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa kushirikiana na Shule za Msingi Kisutu na Mtendeni leo tarehe 30, Oktoba, 2023 wamefanya hafla ya Maadhimisho ya Siku ya Lishe Kitaifa yaliyofanyika katika Shule ya Msingi Kisutu, yenye kauli mbiu inayosema "Lishe Bora kwa Vijana Bqlehe, Chachu ya Mafanikio yao"
Akiongea katika Maadhimisho hayo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Afisa Elimu Msingi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Bw. Hossein Mghewa amesema "Nia ya Siku ya Lishe ni kuelimisha umma kuhusu lishe na utapiamlo kwa Tifa letu hasa kwa watoto na vijana, kwani vijana ndio nguvu kazi ya Taifa letu. Hivyo nawasihi vijana kuacha kula vyakula visivyofaa kwa sababu havina madini na vitamini zinazofaa katika ukuaji zaidi husababisha kupata balehe za mapema hivyo tupendelee kula mbogamboga na matunda, kwa sababu vijana mlio kwenye balehe mnahitaji lishe bora."
Sambamba na hilo Bw. Mghewa ametoa shukrani zake kwa waalimu, wanafunzi na wote walioshiriki katika maandalizi ya Maadhimisho ya siku ya lishe kitaifa na kuwaomba walimu wote wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kuwa na vikundi (clubs) za kuhamasisha lishe bora katika shule zote za msingi.
Aidha, mratibu wa Lishe wa Halmashauri ya Jiji la DSM Bi. Flora Mgimba amesema "Lishe ni jambo la msingi katika makuzi ya mtoto na kijana katika taifa letu ndio maana Serikali yetu iliona umuhimu wa kua na maadhimisho ya siku ya lishe kwa sababu vijana ndio taifa la kesho na vijana ndio nguvu kazi ya Taifa, na tunahitaji vijana wenye Afya njema katika kulijenga taifa letu, lishe Bora inaendana na mazoezi hivyo nawaasa hii elimu mnayoipata mkaipeleke kwa familia zenu na jamii inayowazunguka."
Akiongea kwa niaba ya walimu na wanafunzi, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kisutu Mwl. Elizabeth Massawe amemshukuru mgeni rasmi kwa kushiriki pamoja nao kwani elimu na kuahidi kuendelea kutoa Elimu ya lishe bora kwa wanafunzi kwa njia ya masomo, nyimbo na maigizo.
Maadhimisho ya siku ya lishe yalianza rasmi Julai 2020 ambapo huadhimishwa kila tarehe 30 Oktoba.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.